WAFANYABIASHARA waliokuwa wanafanya shughuli zao soko la Manzese A na B katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,wameiomba serikali kupitia Manispaa hiyo kuharakisha ujenzi wa soko jipya ili waweze kurudi na kufanya shughuli zao kama hapo awali.
Wafanyabiashara hao wameondolewa katika soko hilo kwa ajili ya kupisha ujenzi wa soko la kisasa litakaloendana na hadi ya Manispaa hiyo,kazi inayotarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema,tangu soko hilo lilipovunjwa mwezi Julai,bado ujenzi haujaanza hivyo wana wasiwasi kazi itakuchukua muda mrefu hadi kukamilika,jambo litakalowawia vigumu kuendelea kumudu gharama ya maisha yao.
Aziz Kapakapa alisema,tangu soko hilo lililopo vunjwa wameathirika sana kiuchumi kwani eneo hilo ndiyo walilotegemea kupata riziki zao za kila siku,lakini kwa sasa wanaishi maisha magumu na familia zao.
Ameiomba serikali,kuharakisha kazi hiyo na kujenga soko la viwango ili kuwavutia wafanya biashara kurudi na wateja wengi kwenda kununua bidhaa zitakazopatikana katika soko hilo maarufu soko la wakulima.
Kapakapa,ameipongeza Manispaa ya Songea kuwa na mpango wa kujenga soko la kisasa,lakini ameomba imsimamie kwa karibu fundi au mkandarasi atakayepewa kazi ili kuepuka kujengwa chini ya kiwango kwa kuwa Manispaa ya Songea ndiyo kioo kwa wageni wanafika katika mkoa wa Ruvuma.
Athuman Majimoto mfanyabiashara katika soko la Manzese tangu mwaka 2012 alisema, kuwaondoa katika eneo hilo ni kama uonevu kwao kwa sababu hakuna maridhiano yoyote yaliyofikiwa kati ya Manispaa na wafanyabiashara hao.
Alisema,hawapingi kuondolewa katika eneo hilo lakini Manispaa wangetumia busara kuwashirikisha na kutoa elimu juu ya faida zitakazo patikana kutokana na uwepo wa soko jipya.
Aidha,ameiomba Serikali mara soko litakapokamilika kuwaangalia kwanza wafanyabiashara waliokuwepo awali, badala ya kuwapa nafasi watu wenye fedha ambao hawakuwepo katika soko hilo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Betram Njelekela alisema,serikali imeamua kuvunja soko la Manzese A na B ili kujenga soko la kisasa katika eneo hilo, badala ya kuendelea na soko la lazima ambalo vibanda vyake viliezekwa kwa magunia.
Alisema, mji wa Songea unakuwa kwa kasi kubwa tofauti na miaka kumi iliyopita,na hata idadi ya watu imeongezeka sana, kwa hiyo wanahitaji vitu vizuri na siyo kuendelea kuwa na vitu vya kizamani na mazingira ambayo hayaendani na hadhi ya mji maarufu wa Songea.
Alisema Manispaa ya Songea ndiyo kioo kwa mkoa wa Ruvuma,kwa hiyo ni muhimu kuwa na majengo na miundombinu ya kisasa ambayo yataendana na sifa ya mkoa huo ambao uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa na unaoongoza kwa uzalishaji wa chakula hapa nchini.
Amewataka wananchi hususani wafanyabiashara kuwa wavumilivu, wakati huu ambao serikali inaendelea kukamilisha taratibu za mwisho kwa ajili ya kuanza ujenzi wa soko hilo na baada ya kukamilika watafurahi kutokana na uwekezaji utakaofanyika katika eneo hilo.
“kwa niaba ya mkurugenzi wa Manispaa nawaomba wananchi wa Songea watuamini kwamba sisi ni wataalam, hatufanyi vitu kwa kukurupuka hata kidogo, tunakwenda kujenga soko la kisasa ambalo baadhi yao hawajawai kuliona,nawahakikishia baada ya kukamilika hata wale wanaolalamika watafurahi na kutupongeza”alisema Njelekela.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.