Shule ya sekondari ya wasichana ya Songea (Songea Girls) iliyopo mkoani Ruvuma imeadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1974, ambapo maadhimisho hayo yamelenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kujenga uzio wa shule hiyo.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Jumanne Mwankhoo, ameongoza zoezi la uchangiaji fedha na kufanikiwa kukusanya jumla ya shilingi milioni 1,380,000 papo hapo, huku ahadi ya shilingi milioni 30,520,000 ikitolewa, na kufanya jumla kuwa shilingi milioni 31,900,000, huku wadau wengine wakiahidi kuchangia mchanga tripu nne na mifuko 44 ya simenti.
Kaimu Katibu Tawala amemuagiza Mtendaji wa kata ya Mjini kuhakikisha wanalinda maeneo ya shule kabla uzio haujaanza kujengwa kutokana na uvamizi wa wananchi unaoendelela katika eneo la shule hiyo.
Katika hatua nyingine Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma amezindua chumba cha tehama ambacho kina jumla ya kompyuta 43, ambazo zimetolewa na shirika lisilo la kiserikali linalojulikana kama Camara Education Tanzania ambalo lilitafuta mfadhili kutoka Marekani ambaye ni Rose Code na kufanikisha upatikanaji wa kompyuta hizo.
Ndugu Mwankhoo ameutaka uongozi na wanafunzi wa shule hiyo kwa ujumla kuhakikisha wanazitunza kompyuta hizo ili ziweze kusaidia kwa muda mrefu na kuzitumia kwa manufaa ambayo Serikali na wadau wameyakusudia.
Maadhimisho hayo ya miaka 50 ya shule ya sekondari ya wasichana ya Songea yaliyohudhuriwa na walimu pamoja na wanafunzi waliosoma shuleni hapo miaka ya nyuma, yamelenga kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika shule hiyo ili kuepuka changamoto zinazojitokeza shuleni hapo ikiwa ni pamoja na wizi wa mali za wanafunzi na shule.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.