TAASISI isiyokuwa ya kiserikali ya Saint Teresa Orphans Foundation (STOF) imetoa mchango mkubwa katika sekta ya ustawi wa jamii na afya mkoani Ruvuma.
Mkurugenzi wa STOF Teresa Nyirenda anasema STOF ambayo ilianzishwa mwaka 2001 na inafanyakazi katika nchi mbili za Tanzania na Marekani.
Ili kuhakikisha inatoa mchango wake kikamilifu katika sekta ya Afya,Nyirenda anasema Taasisi hiyo iliamua kuanzisha zahanati ya Mtakatifu Benjamin yenye hadhi ya kimataifa iliyopo Msamala mjini Songea ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya afya jirani na maeneo wanayoishi.
“Zahanati hiIi imedhamiria kutoa huduma bora za matibabu kwa watu wote,hata mimi Mkurugenzi wa STOF na familia yangu yote tukiugua tunapata huduma katika zahanati hii,tumepania kutoa huduma zaidi badala ya kutafuta faid’’,anasisitiza Nyirenda.
Kwa mujibu wa Nyirenda Zahanati ya Mtakatifu Benjamin ilifunguliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 ambapo Kiongozi wa Mbio wakati huo Charles Kabeho aliridhishwa na ubora na vifaa vya zahanati hiyo akisema inakubalika na serikali kwa kuwa na mundombinu bora na ya kisasa.
Anasema Ujenzi wa zahanati ya Mtakatifu Benjamini ulianza mwaka 2012 na kukamilika mwaka 2014 ambapo gharama ya ujenzi huo ni zaidi ya shilingi milioni 468 na kwamba vimenunuliwa vifaa vya kisasa vinavyotumika katika zahanati hiyo.
Anaitaja zahanati hiyo kuwa ina vyumba 19 na kwamba inahudumia wakazi 345 kwa mwezi wanaotoka katika maeneo mbalimbali mkoani Ruvuma.
“Lengo la kujenga zahanati hii ni kusogeza huduma kwa jamii,lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa’’,anasema Nyirenda.
Leonard Mtitu ni Mganga Mkuu wa zanahati hiyo anazitaja huduma ambazo zinatolewa na kituo hicho kuwa ni huduma kwa magonjwa ya maambukizi njia ya mkojo, kichomi, kuhara, malaria, magonjwa ya zinaa na magonjwa mengine.
Anatoa rai kwa wananchi kuitumia zahanati hiyo ambayo inatoa huduma kwa takribani saa nane kwa siku na kwamba zahanati hiyo ina wataalam wenye viwango vya kitaifa na kimataifa.
Anasema kituo hicho kinafanyakazi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na serikali na kwamba zahanati hiyo ina vitanda vya kumpumzisha mgonjwa na sio kulazwa hivyo akipata nafuu anaruhusiwa kwenda nyumbani.
“Zahanati ya St.Benjamini ina wodi nne na vitanda saba,zahanati yetu pia inatoa huduma za bima ya afya’’,anasema Mtitu.
Coletha Carrosi ni Mkazi wa Msamala mjini Songea anasema zahanati hiyo ndiyo kituo anachokitumia kila anapougua kutokana na huduma bora za matibabu ambazo amekuwa anazipata, hivyo anatoa rai kwa wengine kuitumia zahanati hiyo kwa matibabu bora.
Licha ya kutoa huduma za kiafya kupitia zahanati hiyo,STOF pia inaendesha mradi wa lishe kwa watoto yatima,wenye utapiamlo na ambao wazazi wao wameathirika na virusi vya UKIMWI.
Mkurugenzi wa STOF nchini Marekani Teresa Nyirenda anasema mradi umelenga kuhudumia watoto katika Mkoa mzima wa Ruvuma na kwamba mradi wa lishe unaotekelezwa sasa kwa mwaka mmoja unatarajia kuwafikia watoto zaidi ya 200 ndani ya Mkoa.
“STOF inatoa bure maziwa ya unga ya mbuzi kwa watoto yatima,wenye utapiamlo na ambao wazazi wao wameathirika na HIV,natoa rai kwa walezi na vituo vya kulelea watoto yatima kuwasiliana na Taasisi yetu ili kuwapa maziwa hayo bure,’’,anasisitiza Nyirenda.
Hata hivyo analitaja lengo la STOF kutekeleza mradi wa lishe ya maziwa ya mbuzi kwa watoto kuwa ni kuhakikisha mtoto anahusika na ukuaji wa kimwili na kiakili kwa kupata lishe bora sanjari ya kupata huduma za kiafya na kielimu.
Anabainisha zaidi kuwa maziwa ya mbuzi yanafanana kwa ubora na maziwa ya mama ambapo hadi sasa STOF inahudumia watoto wadogo yatima zaidi ya 130 ambao wanapata lishe ya maziwa ya unga ya mbuzi ili kuhakikisha watoto wanaepukana na udumavu ambao unaleta athari kubwa katika ukuaji wa watoto.
Anasisitiza kuwa mradi wa lishe ya maziwa ni endelevu na kwamba hivi sasa wanajipanga kuanzisha mradi wa kufuga mbuzi wa maziwa ambao watatumika kuzalisha maziwa ya mbuzi ambayo ni muhimu kwa watoto.
STOF ni Taasisi binafsi ambayo ilianzishwa mwaka 2001,inafanyakazi katika nchi mbili za Tanzania na Marekani,hadi sasa imehudumia watoto yatima zaidi ya 300 na kuwasomesha kuanzia chekechea,sekondari hadi vyuo vikuu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.