TAASISI ya Saint Teresa Orphans Foundation(STOF) inayofanyakazi mkoani Ruvuma nchini Tanzania na nchini Marekani kupitia mfumo wa TEDNA imeweza kuwapatia vijana mafunzo ya ujasiriamali na kufanikiwa kufungua kampuni zao.
Mkurugenzi wa STOF Teresa Nyirenda anasema Taasisi yake imeamua kuanzisha mfumo wa TEDNA baada ya kubaini kuna kundi kubwa la vijana wamemaliza vyuo vya kati na vyuo vikuu wamekosa ajira.
Nyirenda anasema kupitia TEDNA vijana waliomaliza vyuo vikuu wameunganishwa na kupewa mafunzo na mitaji ili waweze kujiajiri na kuajiri vijana wengine waliokosa ajira.
Vijana kadhaa mkoani Ruvuma kupitia Taasisi ya STOF wamepata mafunzo na mitaji hivyo kufanikiwa kufungua kampuni zao chini ya usimamizi wa TEDNA.
Galus Mpepo ni kijana wa Songea ambaye amelelewa na STOF tangu akiwa na umri wa miaka nane ambapo hivi sasa ni mhitimu wa chuo kikuu ambaye alipata changamoto ya ajira.
Mpepo anasema kutokana na changamoto hiyo STOF iliamua kuwapatia mafunzo na kuwawesha kuanza biashara na kumiliki kampuni yenye uwezo wa kuzalisha nyama za kusindika na kusindika bidhaa mbalimbali kama unga na maharage.
Hata hivyo anasema amejikita zaidi katika kilimo ambacho kitamwezesha kupata malighafi za mashambani kama mahindi,soya,alizeti ambazo anazitumia katika ufungaji wa kuku na nguruwe.
“Hivi sasa natumia muda wangu zaidi katika kuimarisha kampuni yangu ambapo nimeanzia kufanya shughuli za uzalishaji katika eneo la Mlilayoyo wilayani Namtumbo,katika eneo langu kuna sehemu nimelima mashamba na eneo linguine nimefuga mifugo kuku na nguruwe’’,anasema Mpepo.
Kwa upande wake Romana Haule mnufaika wa TEDNA anasema amefanikiwa kuanzisha kampuni ya chakula ambapo hivi sasa anawafanyakazi watatu.
Anaishukuru Taasisi ya STOF kwa kumwezesha mafunzo na mtaji hivyo kufanikiwa kuanzisha biashara hiyo kupitia mfumo wa ujasiriamali wa TEDNA ambapo hivi sasa ameweza kuwatunza watoto wake na kuwalipa mshahara wafanyakazi wake.
Naye Zesco Ngonyani ni mmoja wa vijana waliofanikiwa kuanzisha kampuni ya ujenzi kupitia mfumo wa TEDNA ambapo anasema STOF imemsaidia kumpeleka shule hadi kumaliza kupata mafunzo ya ufundi ujenzi ambapo awali alikuwa anafanyakazi mitaani bila usimamizi madhubuti.
“STOF waliniangalia na kuona mafanikio yangu yanachelewa ndipo,wakanisaidia kuanzisha kampuni ya ujenzi nikiwa na vijana wenzangu,kwa hiyo hivi sasa Napata tenda za kujenga majengo kuanzia msingi hadi kuezeka na umaliziaji wote ikiwemo kupaka rangi’’,anasema Ngonyani
Anasema Kampuni yake ina mafundi bora,wenye uwezo wa hali ya juu na kwamba wanafanya kazi kwa uaminifu mkubwa hali ambayo imesababisha kampuni yao kuaminika na kupata kazi nyingi.
Anasema kampuni yake ina uwezo wa kufanya kazi zote zinazohusika na ujenzi kuanzia kujenga,kuezeka,kupaka rangi,kuchomelea,kuweka umeme,kutengeneza samani na kwamba mteja akikabidhi ramani ya nyumba wao wanamaliza kila kitu na kumkabidhi nyumba iliyokamilika kwa asilimia 100.
Anatoa shukurani kwa STOF kwa kumpeleka shule,kupata mafunzo na kupewa mtaji hali ambayo inamwezesha kuanzisha kampuni ya ujenzi hali ambayo imwezesha kuajiri vijana wengine.
Viviana Komba ni miongoni mwa vijana ambao wamesaidiwa na STOF tangu akiwa na umri wa miaka nane ambapo amesomeshwa hadi elimu ya chuo kikuu katika fani ya ualimu.
Viviana anasema baada ya kumaliza chuo kikuu alikosa ajira hivyo Mkurugenzi wa STOF Teresa Nyirenda alivyoona vijana wengi wanamaliza vyuo na kukosa ajira alianzisha TEDNA ili kuwakuza kifikra na kimtazamo vijana na kuwapatia mitaji ili waweze kufanya biashara na kufungua kampuni zao.
Anasema walipewa mafunzo mbalimbali kabla ya kupewa mitaji ambapo yeye alipata wazo la kuanzisha kampuni ya kutengeneza nepi za watoto kwa kutumia pamba laini ambazo hazina madhara kwa watoto ukilinganisha na nepi za dukani.
Kupitia kampuni yake,Viviana anasema anatengeneza sabuni za maji,dawa za kusafishia masinki,anatengeneza mablankenti ya watoto,mapambo ya shingoni na mkononi,pochi za shanga na vikoi vya kimasai.
“Nina mashine za kisasa zinazoniwezesha kutengeneza bidhaa hizo,lengo langu ni kumiliki kampuni kubwa itakayoajiri watu na kuwasaidia vijana wengine ambao wapo mitaani hawana ajira’’,anasisitiza.
Hata hivyo anasema bidhaa ambazo amezitengeneza baadhi ameshaanza kuuza na kwamba bado bidhaa nyingine zipo kwenye mchakato wa kutengeneza jina la kibiashara ili hatimaye kuziingiza sokoni.
Makala imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.