KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha sekta ya elimu nchini,shirika la Tanzania Development Trust(TDT) na Eucanaid,wamekabidhi vyumba sita vya madarasa vyenye thamani ya Sh milioni 68 kwa shule ya sekondari Mkanona Halmashauri ya wilaya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Mbali na vyumba vya madarasa, mashirika hayo yamekabidhi matundu kumi ya vyoo vya wanafunzi,choo cha walimu,ofisi ya mkuu wa shule na ofisi ya walimu wa shule hiyo ili kuwatia moyo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku na kupunguza uhaba wa baadhi ya miundombinu ya shule hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madarasa hayo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Nanyumbo Mariam Chaurembo,mwakilishi wa TDT &UECANAID Mchungaji Linus Burian alisema,kama wadau wakubwa wa maendeleo wana wajibu wa kuunga mkono juhudi mbalimbali za serikali katika kutatua changamoto ya elimu.
Alisema, katika kata hiyo yenye vijiji sita kwa muda mrefu hakukuwa na shule ya Sekondari na wanafunzi wanaomaliza shule ya msingi walikosa nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari na wachache waliopata nafasi hiyo walilazimika kwenda kusoma shule ya sekondari kata nyingine ya Nanyumbu umbali wa km 38.
Alisema,mahitaji ya shule ya sekondari kwa wavulana na wasichana wa kata hiyo wanaomaliza darasa la saba yalikuwa makubwa, kwa hiyo kama wadau wakaona kuna umuhimu wa kuunga mkono kwa kujenga madarasa hayo.
Linus ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Doyasisi ya Masasi,ameshukuru mashirika hayo yenye makao makuu yake nchini Uingereza na Ubelgiji kuweza kukamilisha ndoto za vijana wengi wa kata hiyo hasa wa kike ambao ndiyo hasa waliongoza kukatisha masomo yao kwa sababu ya kutembea umbali mrefu kutoka katika vijiji vyao kwenda kwenye shule walizopangiwa kuendelea na elimu ya sekondari.
Alisema,kama wadau wa maendeleo wataendelea kushirikiana na serikali kutatua baadhi ya changamoto katika sekta ya elimu,maji,afya na zile zilizopo katika vijiji kwa kukaa na jamii ili kuibua miradi itakayowezesha kupata fedha kutoka kwa wafadhili.
Ameipongeza serikali kwa kuwekeza nguvu kubwa katika ujenzi wa miundombinu katika sekta ya elimu hapa nchini,na kuwaomba wadau mbalimbali kuungo mkono juhudi hizo ili vijana wengi wanaomaliza darasa la saba wapate nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari.
Mwakilishi wa Eucanaid kutoka Ubelgiji Edgar Thielinann alisema, kijiji hicho ni muhimu sana kwao kwa kuwa elimu ni moja ya kipaumbele kikubwa na wamefurahi kuona shule hiyo imeshafunguliwa,ina wanafunzi,walimu na vifaa vya kufundishia.
Alisema,huo ni mwanzo tu na wanajua bado kuna changamoto nyingi kwa kuwa kuna wanafunzi wengine watakuja kusoma katika shule hiyo na kuomba ushirikiano ulioonyeshwa kati ya wananchi,serikali na shirika hilo uendelee.
Kwa upande wake David Gibbons kutoka shirika la TDT la Uingereza alisema,mwaka 2019 alipotembelea kijiji cha Marumba kwa ajili ya kutembelea miradi inayotekelezwa na shirika hilo alipata nafasi ya kufika shule ya Mkanona ambayo majengo yake yalikuwa machache na porini.
Alisema,akiwa na Linus Buriani mwakilishi wa TDT Nchini Tanzania, walijadiliana sana juu ya kuisaidia shule hiyo ili kuongeza idadi ya majengo kwa ajili ya wanafunzi na walimu waliopangiwa kufanya kazi katika shule hiyo.
Hata hivyo,ameshukuru kuona baada ya kurudi Uingereza alipata picha za baadhi ya wananchi wakishiriki katika ujenzi wa shule hiyo kwa kuchimba mitaro,kubeba mawe na wengine kushiriki katika ujenzi ambapo alivutiwa na jitihada hizo za wananchi wa Namijati na kuamua kutafuta wafadhili wengine watakoungana na TDT ili kuongeza idadi ya majengo na miundombinu mingine ya shule.
Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu Mariam Chaurembo,amewashukuru wafadhili shirika la Tanzania Development Trust(TDT) na Eucanaid kusaidia kutatua changamoto katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Alisema,kabla ya kujengwa kwa shule hiyo wanafunzi wanaotoka kata ya Mkanona walilazimika kutembea umbali wa km 38 kwenda shule ya Sekondari kata ya Nanyumbu jambo lililo sababisha baadhi yao kukatisha masomo.
Alisema,kuwepo kwa shule hiyo sasa kumesaidia kupunguza tatizo la kutembea umbali kufuata masomo,utoro na kuongeza taaluma kwa wanafunzi.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya,serikali ya awamu ya sita ilishajenga vyumba vinne vya madarasa kupitia fedha za mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya Covid-19 na itaendelea kufanya hivyo kadri fedha zitakapopatikana.
Amewataka,wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya elimu,badala ya kazi hiyo kuiachia serikali peke yake.
Aidha alisema,serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 itahakikisha inapeleka nishati ya umeme katika shule hiyo ili wanafunzi waweze kusoma hata majira ya siku na walimu wafanye kazi zao wakati wote.
Chaurembo,amewaomba wafadhili hao kusaidia kuboresha(kupeleka) huduma ya maji katika shule hiyo na maeneo mengine ya wilaya ya Nanyumbu ili kupunguza na kumaliza kero ya wanafunzi na jamii kutembea umbali mrefu kutafuta maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku.
Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Ali Yahaya alisema, ujenzi wa shule hiyo ni hatua kubwa ya kimaendeleo katika jimbo la Nanyumbu kwa kuwa itasaidia vijana wa kata ya Mkanona wanaochaguliwa kuanza kidato cha kwanza kuendelea na elimu ya sekondari.
Amewaomba wafadhili na wadau wengine,kuangalia uwezekano wa kujenga mabweni ili wanafunzi wote waishi shuleni badala ya kutokea nyumbani na nyumba za walimu ili kuepuka kupanga uraiani ambapo wananchi wako tayari kushiriki na kujitolea nguvu zao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.