TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imefanikiwa kuokoa fedha za umma zaidi ya shilingi 134 zilizokuwa zimefanyiwa ubadhirifu.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Yustina Chagaka akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa wanahabari mjini Songea katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2019,amesema fedha hizo zilifujwa kwenye vikundi vya ushirika kwa njia nyingine za rushwa.
Chagaka amesema kati ya fedha hizo,zaidi ya shilingi milioni 122 zimewekwa kwenye akaunti maalum ya serikali iliyopo Benki Kuu ya Tanzania(BOT) na kwamba kati hizo zaidi ya shilingi milioni 118 ni marejesho ya iliyokuwa Benki ya wananchi wa Mbinga(MCB).
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma,shilingi 1,908,000 ni marejesho ya fedha zilizokuwa zimefujwa kupitia semina hewa iliyofanyika wilayani Namtumbo na shilingi 1,410,103.80 ni marejesho ya fedha za vipimo(Material Test) zilizofujwa kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya NMB-Makalavati kwenye wilaya ya Madaba.
Fedha zingine zilizookolewa amezitaja kuwa ni ni kiasi cha zaidi ya milioni 12 walizorejesha wananchi kati ya fedha hizo kupitia vyama vya Ushirika-AMCOS,shilingi milioni 9.84,walalamikaji katika Kata ya Kagugu shilingi 145,000 na walalamikaji wilayani Songea shilingi 2,100,000.
“Katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2019 TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imepokea jumla ya taarifa 86 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo mbalimbali,Idara zilizoongoza ni Ardhi malalamiko 16,TAMISEMI 10,Taasisi za fedha 9,Poilisi 7,Elimu 7,Vyama vya Ushirika 6 na Afya 4’’,alisema Chagaka.
Kulingana na Chagaka idadi ya kesi zilizofunguliwa katika kipindi hicho ni 12 ambazo washitakiwa wake wanatoka katika Idara za Elimu,Polisi,Maji,Mifugo,Uvuvi,Serikali ya kijiji na TAMISEMI na kwamba kesi mpya tano zilifunguliwa katika Mahakama mbalimbali mkoani Ruvuma.
TAKUKURU ni chombo kilichopewa dhamana kwa mujibu wa sheria na kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11,2007 ya kuongoza vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 23,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.