TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) ni chombo kilichopewa dhamana kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Sheria hiyo inaongoza vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini ambapo TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imeendelea kutekeleza matakwa ya sheria kupitia majukumu matatu ambayo ni kuzuia rushwa,kuelimisha Umma,kuchunguza tuhuma za rushwa na kushitaki watuhumiwa wanaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Hamza Mwenda anatoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo katika kipindi cha kuanzia Oktoba hadi Desemba 2020 ambapo anasema katika kipindi hicho TAKUKURU Ruvuma ilipokea taarifa 170 kutoka kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali.
Anazitaja taarifa hizo zilipatikana toka Idara mbalimbali,kati ya hizo,Idara ya Ardhi taarifa 29,Taasisi za Fedha 25,TAMISEMI 17,Mahakama 13,Elimu 10,,Biashara 10,Polisi 7,Vyama vya Siasa 7,Ujenzi 4,Bima 3 pamoja na taarifa nyingine toka TANESCO,PSSSF,Kampuni ya Ulinzi,Habari,Maliasili,Afya,Uhamiaji na vyama vya Ushirika.
“Katika kipindi hicho idadi ya kesi zilizoendelea mahakamani ni 11,ambazo washitakiwa wanatoka katika Halmashauri mbili,serikali za vijiji vinne,Idara ya Elimu watatu na Idara ya Afya washitakiwa wawili’’,anasema Mwenda.
Hata hivyo Mwenda anasema katika kipindi hicho,kesi tatu zilikamilika na kutolewa uamuzi na mahakama ambapo kati ya kesi hizo,kesi moja iliyokuwa inaendeshwa wilayani Nyasa,mshitakiwa alipatikana na hatia na alihukumiwa kulipa faini ya shilingi 500,000 na kesi mbili washitakiwa waliachiwa huru.
Mkuu wa TAKUKURU Ruvuma anasema katika kipindi cha miezi mitatu,Taasisi hiyo imeokoa fedha kiasi cha Zaidi ya shilingi milioni 50 kutokana na uchunguzi mbalimbali uliofanyika.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 27,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.