TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imekagua miradi mbalimbali ya Zaidi ya shilingi bilioni tano katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi 2022.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa miezi mitatu ya Taasisi hiyo kwa wanahabari mjini Songea,Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Janeth Haule,amesema TAKUKURU imefuatilia miradi hiyo ikiwemo fedha za utekelezaji miradi ya maendeleo kupitia UVIKO 19.
Ameitaja miradi iliyofuatiliwa kuwa ni ujenzi wa vyumba nane vya madarasa katika shule za sekondari Ruhuwiko,Mbambi,Ruanda na Mbinga Girls zilizopo katika wilaya ya Mbinga.
“TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma katika kipindi cha Januari hadi Machi 2022,imeweza kutekeleza majukumu yake ya uchunguzi na kufanikiwa kupokea jumla ya taarifa mpya 45 za malalamiko mbalimbali,kati ya hayo,malalamiko 33 yalikuwa na viashiria vya rushwa na yote yalifanyiwa uchunguzi wa awali’’,alisisitiza Haule.
Hata hivyo amesema kwa upande wa mashtaka katika kipindi cha miezi mitatu,TAKUKURU Ruvuma imeweza kufungua kesi moja ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Wilaya ya Mbinga inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na kufanya jumla ya kesi sita kuendeshwa mahakamani.
Kwa upande wa uzuiaji Rushwa,Naibu Mkuu wa TAKUKURU huyo amesema Taasisi yake imefanikiwa kufanya uchambuzi wa mifumo sita kuhusu utendaji kazi wa Wakala wa Manunuzi ya Serikali (GPSA) na Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (TEMESA).
Hata hivyo amesema viashiria vya rushwa ya ngono katika sekta ya elimu vimejitokeza katika Halmashauri za Manispaa ya Songea,Halmashauri za Wilaya ya Songea,Tunduru na Namtumbo.
Matarajio ya TAKUKURU Ruvuma katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ameyataja kuwa ni pamoja na kuendelea kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wale wote watakaokutwa na tuhuma za vitendo vya rushwa na kuwafikisha mahakamani.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari,Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Aprili 28,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.