Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma imeokoa kiasi cha fedha Shilingi Milioni 102,968,122/= ambazo zimepatikana baada ya chunguzi mbalimbali kufanyika.
Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Owen Jasson, wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Marchi 2021 kwa Waandishi wa Habari iliyofanyika katika ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma tarehe 28 Aprili 2021.
Jasson alisema katika kipindi cha miezi mitatu, Taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa fedha kiasi cha jumla ya Shilingi Milioni 102,968,122/= ambayo imeokolewa kutokana na chunguzi zilizofanyika kwenye vyama vya ushirika (SACCOS) Wilaya ya Songea, Mbinga, Namtumbo, Tunduru na Nyasa.
Jasson alibainisha kuwa fedha hizo zimetokana na marejesho ya madeni kutoka kwenye vyama mbalimbali vya ushirika katika mkoa wa Ruvuma ikiwemo na SACCOS ya walimu (Tunduru), Nambawala AMCOS (Nyasa), Kurugenzi SACCOS (Mbinga), SACCOS (Songea) pamoja na Libango AMCOS (Namtumbo).
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho tajwa, Taasisi hiyo imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 13 Mkoa wa Ruvuma ambayo ni ujenzi wa miundo mbinu ya maji, barabara, elimu na huduma za vikundi, inayotekelezwa katika Wilaya zote Mkoani Ruvuma yenye thamani Zaidi ya Shilingi Bilioni moja ikiwemo mradi wa ujenzi wa nyumba 7 za watumishi wa Wilaya ya Madaba.
Aliongeza kuwa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imefanikiwa kufanya semina na mikutano ya hadhara sehemu mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii juu ya mapambano dhidi ya Rushwa, na kuimarisha klabu za wapinga Rushwa katika shule za msingi na sekondari, Jasson ‘Alisema’.
Aidha, amewashukuru Wananchi kwa kusaidia Taasisi hiyo katika kutoa taarifa kuhusiana na vitendo vya Rushwa kupitia vyanzo mbalimbali ambapo wamefanikisha kupokelewa kwa taarifa 133 katika kipindi hicho cha Januari hadi Marchi 2021.
TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imejipanga kuendelea kuelimisha jamii kupiga vita Rushwa kwa kuwafahamisha madhara ya kutoa na kupokea Rushwa, kutoa taarifa mapema juu ya vitendo vya Rushwa, kuwa tayari kutoa ushahidi pale inapohitajika pamoja na kuendelea kufuatilia miradi ya maendeleo linayoendelea kutekelezwa katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2021.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.