Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limeendelea na kampeni yake ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya umeme, utunzaji wa miundombinu, na utaratibu wa kuomba huduma hiyo muhimu. Kampeni hii inatekelezwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kijiji cha Mkurumusi, Kata ya Mpitimbi.
Katika ziara hiyo, wananchi walipatiwa mafunzo kuhusu njia bora za kutunza miundombinu ya umeme na kujiepusha na vitendo vya hujuma kama wizi wa mafuta ya transfoma na nyaya za umeme aina ya kopa. Aidha, walipewa maelekezo ya jinsi ya kuomba umeme kwa njia za kidigitali kwa kutumia simu janja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Afisa Habari na Uhusiano wa TANESCO Ruvuma, Allan Njiro, alisisitiza kuwa kabla ya kuomba umeme, ni lazima nyumba ziwe na wiring sahihi na ziwe ndani ya maeneo yenye nguzo zinazofikika. Alieleza kuwa gharama ya kupata umeme kwa wakazi wa vijijini ni shilingi 27,000 kwa njia moja, huku gharama ya njia tatu kwa matumizi ya viwanda ikiwa shilingi 139,000, na wakazi wa mijini wakitakiwa kulipia shilingi 321,000.
Kaimu Afisa Habari na Huduma kwa Wateja, Emma Ulendo, alieleza kuwa umeme ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo ni muhimu wananchi kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote muhimu ili kupata huduma hiyo kwa urahisi. Pia, alibainisha kuwa serikali na TANESCO wanaendelea na mpango wa kuhakikisha kila mwananchi, hata walio nje ya kilomita 30, wanapata umeme kwa gharama nafuu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mkurumusi, Casian Joseph Kayombo, akiwasilisha maombi kwa niaba ya Diwani wa Kata ya Mpitimbi, Mheshimiwa Issa Kindamba, aliiomba TANESCO kuwaharakishia wakazi wa eneo hilo huduma ya umeme. Pia, aliipongeza serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Songea Vijijini, Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwa juhudi zao katika kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika.
Wananchi wa Mpitimbi wamepokea kwa furaha taarifa za kuletwa kwa umeme katika maeneo yao na wameahidi kushirikiana na TANESCO kulinda miundombinu. Aidha, wameomba serikali kuharakisha utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha kila kaya inanufaika na huduma hiyo muhimu kwa maendeleo yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.