Zaidi ya tani 1,271 za kahawa zimezalishwa na kukusanywa kupitia Chama cha Msingi cha Ushirika cha Liyombo Amcos katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025, huku wakulima wakinufaika kwa kupata kiasi cha Shilingi bilioni 10.96. Huu ni uzalishaji mkubwa zaidi kuwahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2019.
Katibu wa Chama cha Liyombo Amcos, Angelina Nchimbi, alisema kuwa ongezeko hilo limekuja baada ya jitihada za pamoja kati ya chama na wakulima, ikilinganishwa na msimu wa 2023/2024 ambapo walizalisha tani 309 tu zenye thamani ya Shilingi bilioni 1.58. Alibainisha kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani umeleta manufaa makubwa kwa wakulima na kusaidia kupata masoko yenye ushindani.
Mwenyekiti wa chama hicho, Joseph Mbele, alisema kuwa wamekuwa wakipata mikopo ya pembejeo kupitia Ofisi ya Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma. Alifafanua kuwa msimu wa 2023/2024 walikopeshwa Shilingi milioni 180 na msimu wa 2024/2025 wameidhinishiwa mkopo wa Shilingi milioni 350, fedha zilizosaidia kununua mbolea, dawa na kulipia awamu ya kwanza ya malipo kwa wakulima.
Aidha, Mbele alisema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa Amcos, wakulima walikuwa wakikumbwa na changamoto za kiuchumi kutokana na gharama kubwa za pembejeo na kukosa sehemu ya kuhifadhi kahawa, lakini kwa sasa wamepata mwelekeo mzuri kupitia chama hicho na ushirikiano na Bodi ya Ushirika ya Mbinga (Mbifacu).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kitengo cha uzalishaji wa Amcos hiyo, Yukundus Hyera, alisema kuwa ruzuku ya pembejeo iliyotolewa na Serikali ya awamu ya sita imeboresha hali ya mashamba na kuongeza uzalishaji mara mbili zaidi. Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa pembejeo kwa bei nafuu, hali ambayo imeleta mafanikio makubwa kwa wakulima wa kahawa wilayani Mbinga.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.