WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma,umewahakikishia wakazi wa wilaya za Mbinga na Nyasa wanaotumia barabara ya Amanimakoro-Ruanda yenye urefu wa kilometa 35 kuwa,ujenzi wa barabara hiyo unaendelea na itakamilika mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Saleh Juma, baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami na Mkandarasi kampuni ya China Railway Sevent Group(CRSG) kwa gharama ya Sh.bilioni 60.4.
Amesema,barabara ya Amanimakoro-Ruanda ni ya kimkakati na muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla kwani inaunganisha wilaya ya Mbinga,Nyasa na mkoa jirani wa Njombe na inatumika kusafirisha makaa ya mawe kutoka Ruvuma kupeleka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Saleh kwa sasa kazi ya ujenzi inaendelea vizuri na kwamba matarajio ya Serikali barabara hiyo itakamilika haraka ili wananchi waweze kuitumia kwenye shughuli zao za usafiri na usafishaji.
Amesema,barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kitai-Ruanda hadi Lituhi kuelekea Mbambabay wilayani Nyasa kupitia Bandari ya Ndumbi,ambapo Serikali iko katika maandalizi ya kujenga kipande kingine kutoka Ruanda hadi Lituhi kwa kiwango cha lami.
“kimsingi kazi inayofanywa na mkandarasi ni kuandaa lea ya kwanza na pili kabla ya kuweka lami,mpango wetu kwa mwaka huu 2024 tuwe na lami yenye urefu wa angalau kilometa tano,nachukua nafasi hii kuwaeleza wananchi wa mkoa wa Ruvuma kwamba, Mkandarasi yuko saiti na kazi inaendelea"alisema Saleh.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha zilizowezesha ujenzi wa barabara hiyo kuendelea na kuhaidi kumsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi kazi kwa wakati kwani kuwa barabara hiyo inategemewa sana kuharakisha maendeleo na uchumi wa mkoa wa Ruvuma.
Msimamizi wa kitengo cha ndani kutoka TANROADS Mkoa wa Ruvuma Andrew Sanga amesema,mradi huo unahusisha ujenzi wa madaraja makubwa manne kati ya madaraja hayo, matatu ujenzi wake unaendelea ambapo moja limekamilika.
Kwa mujibu wa Sanga,ujenzi wa daraja la pili uko hatua za mwisho na mkanadarasi anamalizia kufunga nondo kabla ya kumwaga zege juu,na mategemeo ya wakala kwamba ujenzi wa madaraja yote yatakamilika kwa wakati.
Meneja mradi wa Kampuni yaCRSG amesema,kazi ya kipande cha barabara chenye urefu wa kilometa tano inaendelea vizuri na itakamilika ifikao mwezi Fabruari mwakani.
Baadhi ya wananchi,wameipongeza Serikali ya awamu ya sita kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo ambayo inakwenda kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kurahisisha usafiri kati ya vijiji vya kata ya Amanimakoro na maeneo mengine ya wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.