WAKALA wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Ruvuma, imeanza kufanya matengenezo makubwa katika barabara zake zilizoharibika kutokana na mvua za masika na shughuli nyingine za kibinadamu katika maeneo mbalimbali.
Hayo yamesemwa na msimamizi wa mradi wa matengenezo ya barabaraya Songea-Tunduru Mhandisi Godfrey Robbi wakati akikagua kazi ya matengenezo ya barabara hiyo eneo la Mingwea wilayani Namtumbo.
Robi alisema,wameanza kufanya matengenezo ya barabara hiyo katika maeneo yote korofi kabla ya mvua za masika ili kuruhusu barabara hiyo kuendelea kutumika kama kawaida katika shughuli mbalimbali za usafirishaji na uchumi.
Alisema, katika barabara hiyo inayounganisha mikoa ya Mtwara-Lindi na Dar es slaam baadhi ya maeneo yake yameharibika kutokana na sababu mbalimbali na Tanroads inafanya matengenezo ili kuhakikisha hakuna shughuli za kiuchumi zinazosimama.
Mhandisi Robbi, ameyataja maeneo yaliyoanza kufanyiwa matengenezo ni Mingwea kwa kurudisha tabaka la lami na eneo la Kaleo kwa kufikia korongo kubwa lililoanza kutishia usalama wa barabara.
Alisema,tatizo la kuharibika kwa barabara hiyo kumetokana na aina ya udongo na maji yanayopita chini ya barabara kutokana na mvua zilizonyesha kwa wingi katika maeneo hayo korofi.
Amewatoa hofu wananchi hasa watumiaji wa barabara hiyo,kuwa na matumaini kwa kuwa mkandarasi yupo eneo la mradi anaendelea na kazi ya kurudisha maeneo hayo katika hali yake ya kawaida.
Alisema, kazi ya matengenezo ya barabara hiyo itakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Julai au mwanzoni mwa mwezi Agosti, kabla ya kuendelea na matengenezo ya barabara kongwe ya Songea-Njombe ambayo imeshachakaa kutokana na kujengwa kwa muda mrefu.
Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni ya OVANS CONSTRUCTIONS LTD inayofanya matengenezo ya barabara hiyo Mhandisi Azimio Mwapongo alisema, changamoto kubwa katika baadhi ya maeneo ya barabara hiyo ni kuwepo kwa maji mengi chini ya ardhi.
Alisema baada ya kubaini tatizo hilo, katika matengenezo ya sasa wameweka mfumo maalum chini ya ardhi ambao hauruhusu maji kukaa, na barabara hiyo itaweza kudumu kwa muda mrefu bila kufanywa matengenezo yoyote .
Ameongeza kuwa,kutokana na matengenezo yanayofanyika ana uhakika tatizo hilo halitarudia tena kwa kuwa kampuni ya Ovans Construction Ltd ina uzoefu mkubwa na wa muda mrefu katika miradi ya ujenzi wa barabara za lami hapa nchini.
Aidha,ameiomba Serikali kupitia TANROADS kujenga mizani kipande cha barabara ya Namtumbo hadi Tunduru ili kudhibiti uzito wa magari yanayopita katika barabara hiyo kwa kuwa madereva wana tabia ya kuongeza mizigo mara baada ya kupitia mizani ya Songea.
Mmoja wa madereva wa magari makubwa Denis Mbawala, ameishukuru Tanroads mkoa wa Ruvuma kwa uamuzi wa kufanya matengenezo makubwa hayo na kuipongeza kampuni ya Ovans Contructions Ltd kwa kazi nzuri inayofanya katika matengenezo ya barabara na miradi mbalimbali katika wa mkoa wa Ruvuma .
"kama mtumiaji wa barabara hii naishukuru Tanroads mkoa na Mkandarasi Kampuni ya Ovans kwa kazi nzuri inayofanya,nina uhakika matengenezo yanayofanyika hii barabara itaendelea kudumu kwa muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo"alisema.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.