WAKALA wa barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma,imekamilisha kazi ya kuimarisha daraja la mto Muhuwesi wilayani Tunduru ambalo liliathirika na mvua za masika na kusababisha taharuki kwa watumiaji wa daraja hilo.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Saleh Juma amesema,kwa sasa daraja hilo ni salama na haliwezi kusogea tena kama ilivyotokea hapo awali, na amewatoa hofu watumiaji hasa wenye magari kuhusu uimara wa daraja hilo linalounganisha mikoa ya Ruvuma,Lindi na Mtwara.
Amezitaja kazi nyingine zilizofanyika,ni kuziba mashimo makubwa kwenye barabara inayoingia katika daraja hilo yaliyosababishwa na maji ya mvua kupita chini ya barabara na kukatika kwa sehemu ya lami.
Amesema, katika eneo hilo barabara imemeza maji na kusababisha ifumuke,lakini tayari TANROADS kwa kumtumia Mkandarasi Kampuni ya Ovans Constructions Ltd imefanikiwa kuziba mashimo yaliyojitokeza.
“katika eneo hili magari yanayopita yalikuwa yanakwama na kusababisha adha kubwa,lakini tayari serikali kupitia TANROADS imefanya matengengezo ya haraka na sasa hali ni shwari”alisema.
Kwa upande wake Mhandisi wa Kampuni ya Ovans Constructions Ltd Azimio Mwapongo amesema, katika eneo hilo kulitokea changamoto ya maji kutokea chini kuja juu ya barabara na kusababisha lami kukatika.
Kwa mujibu wa Mwapongo,kazi zilizofanyika ni ulazaji wa mabomba chini ya ardhi kwa ajili ya kunyonya maji kutoka chini na kuyapeleka nje ili yasikae tena pamoja na kurudishia tabaka la lami.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.