SHIRIKISHO la Taasisi Ndogo za Fedha Tanzania (TAMFI) limeingia makubaliano na Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) kuona namna bora ya kuongeza kasi ya kuwekeza katika matumizi ya nishati jadidifu nchini Tanzania.
Uongozi wa pande hizo mbili wakizungumza katika kongamano la siku mbili kuhusu uwekezaji katika nishati jadidifu, wamesema kumekuwepo na ongezeko la matumizi ya nishati hiyo hivyo ni lazima hatua zichukuliwe kuhakikisha kwamba wananchi wanapatiwa uwezo wa kuipata na kutumia.
Katibu Mtendaji wa Tamfi, Winnie Terry, akizungumza alisema: "Nishati mbadala sio tu inatakiwa kwa siku zijazo; ni ya sasa. Ushirikiano wetu na Tarea ni ushahidi wa kujitolea kwetu kufanya nishati mbadala kupatikana kwa wote."
Naye Katibu Mtendaji wa Tarea, Dk Matthew Matimbwi alisema: “Kupanda kwa takwimu za kuunganishwa kwa nishati ya jua, inayofikia asilimia 30.4 ya umeme wa majumbani Tanzania, si takwimu tu, bali ni matumaini na maendeleo.
“Makubaliano yetu na Tamfi yataongeza takwimu hizi na kuhakikisha mustakabali endelevu kwa Watanzania wote."
Tamfi na Tarea zimekubaliana kuhakikisha kuwa wajasiriamali chipukizi na wanajamii wanapata huduma sahihi za kifedha ili kuwezesha kupata nishati jadidifu.
Katika hatua kubwa ya kuziba pengo la ujuzi wa nishati ya jua, kituo cha mafunzo cha Don Bosco kinaendesha programu zinazolenga kupata mafundi wa nishati ya jua.
Alfred Dalasia - Ofisa Programu, Don Bosco, alisema katika kuimarisha sekta ya nishati mbadala wamewezesha mafunzo kwa vijana zaidi ya 1,000.
Nayo Taasisi ya Nishati na Maisha kwa Jamii (E-LICO), imesema kama taifa juhudi lazima ifanyike juhudi kufikia kiwango cha juu cha matumizi ya nishati jadidifu kwa ajili ya kuinua kijamii vijijini Afrika.
“Tunasaidia kwa kukopesha vifaa vya nishati ya jua kwa wakulima, kuwasaidia katika kuchimba visima na kuendesha mifumo yao ya umwagiliaji. Mradi wetu wa sasa uko Iringa na Dodoma—shukrani kwa msaada wa wafadhili—lengo letu ni kupanua wigo wetu nchini Tanzania na labda hata Afrika,” alifafanua Tulibako Mwansasu kutoka Taasisi ya E-LICO.
Alisema lengo la E-LICO sio tu kuwasha taa nyumbani bali ni kuendesha biashara za wakulima, wafugaji, na wavuvi.
"Tunawapa zana za umeme na kuwaelimisha jinsi ya kuzitumia. Na kwa matatizo ya vifaa, tunawaunganisha na wahandisi wa ndani. Tunatoa pia suluhisho kama vile friji zinazoendeshwa kwa nishati ya jua, zinazosaidia kuhifadhi bidhaa muhimu kama samaki, nyama, na maziwa katika maeneo ambayo umeme ni vigumu kupatikana.” alisema.
Tanzania ina uwezo mkubwa wa nishati endelevu, na rasilimali nyingi za jua, upepo, maji, na jotoardhi. Serikali ya Tanzania imejiwekea lengo la kuzalisha 50% ya umeme wake kutoka vyanzo vya nishati endelevu ifikapo mwaka 2030.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.