Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Tanzania Project, Wilaya ya Nyasa limetoa msaada wa vifaa vya kunawia maji vyenye Thamani Ya Tsh 3,710,000/= kwa Wananchi wa Wilaya ya Nyasa ili kujikinga na Virusi vya Corona .
Vifaa hivyo vimekabidhiwa leo na Mratibu wa Shirika hilo Wilayani Nyasa Denis Katumbi kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela Chilumba ili, avigawe kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa ili wachukue tahadhari ya kukabiliana na Ugonjwa wa Corona kwa kunawa mikono .
Akikabidhi vifaa hivyo Bw. Katumbi alifafanua kuwa Shirika la Tanzania project linawajali wananchi wa Wilaya ya Nyasa na amepokea msaada huo kutoka makao makuu ya Shirika hilo yaliyopo Nchini Norway ili kuwasaidia na kuwawezesha watanzania walioko Nyasa kujikinga na kuchukua Tahadhari dhidi ya Ugonjwa Hatari wa Corona ambao hauna dawa.
Alivitaja vifaa alivyochangia kuwa ni, Ndoo na mifuniko yake ya kunawia maji mia moja arobaini na nane (148) na sabuni za kunawia, za nusu lita , mia tano sabini na mbili (572) na kutoa wito kwa wananchi wote wa Wilaya ya Nyasa kufuata maelekezo ya wataalamu wa Afya pamoja na Viongozi wa Serikali ili waweze kujikinga na Ugonjwa wa Corona.
Akipokea Msaada huo kwa niaba ya Wananchi wa Wilaya ya Nyasa,Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela Chilumba amelishukuru Shirika hilo kwa kutoa Msaada kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa kwa kuwa ni Msaada ambao ulikuwa ukihitajika,lakini alisema shirika hilo limeonyesha ni jinsi gani linawapenda wananchi wa Wilaya ya Nyasa hivyo aliwataka wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuhakikisha wanakuwa na sehemu nyingi za kunawa mikono, ili kujikinga na Ugonjwa wa Corona.Aidha alisema atagawa katika Taasisi zote na sehemu zenye mahitaji ya Vifaa hivyo.
“Nachukua fursa hii kuwapongeza sana ndugu zangu wa Tanzania Project Toka Nchini Norway kwa kujali Afya za wananchi wa Nyasa msaada waliotupatia ni mkubwa mno na ni wakati muafaka wa mapambano dhidi ya Corona hivyo tutahakikisha tunagawa katika masoko yote Wilayani hapa na kuhakikisha tunatoa elimu kwa wananchi wote wilayani hapa ili kupambana na Ugonjwa wa Corona”alisema Bi Chilumba.
Kwa kuanzia Leo amegawa vifaa hivyo katika Soko la Kilosa, Soko la Mbamba-bay na madereva wa Bodaboda wa Stand ya Mbamba-bay Wilayani hapa.
Imeandaliwa na
NETHO C.SICHALI
KAIMU AFISA HABARI
Nyasa dc 0767417597
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.