WAKALA wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,imeanza kazi ya kufungua barabara mpya katika maeneo mbalimbali wilayani humo ili kuchochea kasi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Miongoni mwa barabara mpya zilizofunguliwa ni Mandepwende- Masuguru yenye urefu wa kilomita 15 kwa gharama ya Sh.milioni 69 ambayo imepita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na biashara.
Kaimu meneja wa Tarura wilayani Namtumbo Mhandisi Albert Mtimba alisema,kabla ya kufunguliwa kwa barabara hiyo wananchi wa maeneo hayo walipata shida kubwa ya kusafirishaji mazao kwenda sokoni.Kwa mujibu wa Mtimba ni kwamba,hali hiyo iliwaathiri sana wananchi wa maeneo hayo katika jitihada zao za kujikomboa na umaskini kwa kuwa walilazima kuuza mazao yakiwa shambani tena kwa bei ndogo ili kuepuka gharama ya usafirishaji.
Alisema,awali haikuwepo barabara ya uhakika inayounganisha kata ya Rwinga na Masuguru kwa kutumia vyombo vya moto kama magari na pikipiki,badala yake wananchi walilazimika kutembea kwa miguu wanapohitaji kwenda katika maeneo mengine kufuata huduma za kijamii.
Alisema,kutokana na jitihada za Tarura kwa sasa barabara hiyo inapitika na imeanza kutumika kusafirisha mazao na kuwataka wananchi kuitumia kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mkazi wa kijiji cha Masuguru Hamis Undole alisema,awali barabara hiyo ilikuwa changamoto kubwa pindi wanapotaka kusafiri kwenda maeneo mengine kufuata huduma mbalimbali za kijamii.
Undole,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini Tarura kufungua barabara mpya inayounganisha maeneo yenye uzalishaji na masoko.
Mwanahidi Abbas mkazi wa kata ya Rwinga alisema,awali barabara hiyo ilikuwa na mashimo mengi na wakati wa masika haikuweza kupitika kwa urahisi kutokana na mashimo yaliyokuwepo katikati ya barabara kujaa maji na hivyo kusababisha kero kubwa.
Alisema,kwa sasa barabara hiyo ni ni rafiki na wameanza kuitumia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kusafirisha mazao ya kilimo.
Abbas,ameipongeza serikali kwa kazi nzuri iliyofanya kufungua barabara hiyo ambayo itasaidia sana kuharakisha maendeleo yao na kukua kwa uchumi wa wilaya ya Namtumbo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.