WAKALA wa Barabara mijini na vijijini(TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma imeidhinishiwa shilingi milioni 789 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Meneja wa TARURA katika Halmashauri hiyo Mhandisi John Ambrosi amesema Halmashauri hiyo ina mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 1057 kati ya hizo,barabara za lami ni kilometa 13.77,kilometa 250 ni barabara za changarawe na barabara za udongo ni zaidi ya kilometa 700.
“Katika mwaka wa fedha 2020/2021 TARURA tunatekeleza mikataba sita ya ujenzi yenye thamani ya shilingi bilioni 1.396,kati ya hizo shilingi milioni 701 ni kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Muhukuru na fedha inayobakia ni kwa ajili ya matengenezo ya barabara’’,alisema.
Hata hivyo amesema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 TARURA ilikuwa na mradi wa ujenzi wa daraja la Muhukuru ambao unatekelezwa katika mwaka wa fedha 2020/2021.
arabara’’,alisema.
Amesema utekeleza wa miradi hiyo ulianza Agosti 2020 na kwamba hadi kufikia Novemba 2020 jumla ya miradi minne kati ya sita ilikuwa imetekelezwa ambapo hadi kufikia Juni mwaka huu miradi yote inatarajiwa kukamilika kwa asilimia 100.
Hata hivyo amesema licha ya jitihada zinazofanywa na TARURA kuimarisha barabara,madaraja na vivuko,kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazoathiri miundombinu zikiwemo magari yenye uzito mkubwa na mvua za masika zinazoanza Novemba hadi Aprili kila mwaka.
Baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Kijiji cha Litowa wanaishukuru TARURA kwa kuwasaidia kukarabati kivuko kinachounganisha kitongoji cha Goliama na Litowa .
Hata hivyo Christina Njovu na Egno Mwalongo wamesema kivuko hicho kimekuwa kero kwao kwa sababu magari hayawezi kuvuka pia kinahatarisha usalama wao hivyo wanaiomba serikali kuwajengea daraja la kudumu.
Akizungumzia kero ya vivuko hivyo ,Meneja wa TARURA Mhandisi Ambrosi amesema wanatambua changamoto hiyo ambapo hivi sasa bado hawajapata fedha ya kujenga daraja la kudumu.
Amesema TARURA imejenga kivuko cha mbao chenye urefu wa kilometa 21,na kwamba wamekuwa wanakifanyia matengenezo ya mara kwa mara wakati serikali inatafuta fedha za kujenga daraja la kudumu ili kumaliza kero hiyo kwa wananchi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 24,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.