WAKALA wa barabara za vijijini na mijini Tanzania(Tarura),imeanza ujenzi wa barabara za lami katika mitaa mbalimbali ya mji wa mdogo wa Mbambabay wilayani Nyasa unaotajwa kuwa mji pekee wa kitalii mkoani Ruvuma.
Meneja wa TARURA wilayani Nyasa Thomas Kitusi amesema,ujenzi wa barabara za lami ulianza mwaka wa fedha 2022/2023 kwa lengo la kuboresha na kupandisha adhi ya mji huo wenye vivutio vingi vya kitalii ikiwemo ziwa Nyasa na fukwe za kitalii zinazohitaji kuendelezwa.
Alisema,TARURA ilipokea jumla ya shilingi milioni 500 kutoka mfuko wa Jimbo ambapo fedha hizo zimeleta mabadiliko makubwa,hasa ikizingatiwa sehemu kubwa ya barabara za mitaa katika mji huo zilikuwa za udongo.
Alisema kabla ya ujenzi wa barabara za lami, wananchi walipata shida ya kupita kwenye barabara za mitaa zenye tope na kusababisha kero na usumbufu mkubwa pindi wanapotaka kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kwa mujibu wa Kitusi,kero hiyo sasa imekwisha na wananchi wa Mbambabay wameanza kupita kwenye barabara nzuri zilizojengwa kwa lami zilizobadilisha muonekano wa mji huo mkongwe hapa nchini.
Kitusi,amewataka wananchi wa Mbambabay na maeneo mengine kulinda na kutunza barabara hizo na kuacha kutupa taka kwenye mifereji na kuwa walinzi wa miundombinu ikiwemo taa zilizofungwa ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na waweze kuzitumia katika shughuli za maendeleo.
Alisema,ni wajibu kila mmoja kuhakikisha anakuwa mlinzi wa miundombinu hiyo kwani fedha zilizotumika katika ujenzi huo zinatokana na kodi zao ambazo zingeweza kupelekwa katika maeneo mengine hapa nchini.
Baadhi ya wananchi wa mji wa Mbambabay,wameishukuru serikali kwa kujenga barabara za lami ambazo zimesaidia kumaliza kero ya kutembea kwenye tope hasa wakati wa masika na kurahisisha mawasiliano.
Dotto Makungulu mkazi wa kijiji cha Ndengele alisema,kujengwa kwa barabara za lami katika mitaa mbalimbali ya mji huo,kumepandisha adhi ya mji wa Mbambabay na kuongeza thamani ya nyumba zao.
Agnes Chimatila,amewapongeza wataalam wa Tarura kwa kusimamia ujenzi wa barabara hizo ambazo zimesaidia kurahisisha mawasiliano katika mitaa mbalimbali za mji huo na kuiomba serikali kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami katika maeneo mengine ambayo bado kuna changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara za uhakika.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.