AWAMU ya tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) inatarajia kuzifikia kaya masikini zaidi ya milioni 1.4 zinazokadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni saba kote nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga wakati anafungua mafunzo ya siku sita ya timu maalum ya wawezeshaji 25 kutoka Halmashauri za Madaba na Songea wilayani Songea yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Ushirika mjini Songea.
Mwamanga amesema wawezeshaji hao watahusika na utekelezaji na usimamizi wa miradi ya kutoa ajira za muda kwa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF Awamu ya tatu katika kipindi cha pili.
“Miradi ya kutoa ajira za muda inalenga kutoa ajira kwa kaya masikini wakati wa kipindi cha hari ili wanakaya hao wasiweze kuuza rasilimali walizonazo kwa ajili ya kupata fedha na kuwezesha ajira kwa kaya ili kuongeza kipato hivyo kupunguza umaskini’’,alisema.
Hata hivyo amezitaja kaya zitakazoshiriki utekelezaji wa miradi hiyo ni zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi na wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 65.
Mwamanga amesema katika kipindi cha kwanza cha mpango wa kunusuru kaya masikini jumla ya miradi 9,440 ya kutoa ajira za muda ilitekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.19 kati ya hizo shilingi bilioni 83.3 zilitumika kwa kulipa ujira wa walengwa na shilingi bilioni 35.7 kwa ajili ya vifaa vya miradi na usimamizi.
Kwa upande wake Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka TASAF Makao Makuu Frank Antony amelitaja lengo la mafunzo hayo kuwa ni kujenga uwezo wa timu za watalam ngazi ya Halmashauri za Songea na Madaba kuhusiana na uibuaji,uandaaji,utekelezaji na usimamizi miradi ya kutoa ajira za muda kwa walengwa ngazi ya jamii.
Amesema mafunzo hayo ya nadharia na vitendo ya siku sita ambayo yametolewa kwa wawezeshaji 25 toka Halmashauri mbili za Madaba na Songea yatawapelekea maarifa jumla ya walengwa wa TASAF 5,400 kati yao walengwa 3,800 toka Halmashauri ya Songea na walengwa 1,600 toka Madaba.
“Baada ya mafunzo haya tunategemea wawezeshaji watakwenda kuwasaidia walengwa ngazi ya jamii kuibua miradi ngazi ya jamii yenye tija na itakayoonesha thamani ya fedha’’,alisisitiza Antony.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Athuman Nyange ameitaja miradi iliyotekelezwa katika kipindi kilichopita kuwa ni uboreshaji wa visima vya asili,ujenzi wa vivuko vya watembea kwa miguu,uchimbaji mabwawa ya samaki na uanzishwaji vitalu vya miche ya miti.
Nyange ametoa rai kwa wawezeshaji,baada ya mafunzo kuibua miradi yenye tija na yenye kuonesha thamani ya miradi kwa awamu ya pili.
Naye Vitalis Jarando Mwezeshaji aliyepata mafunzo hayo toka Halmashauri ya Wilaya ya Songea amesema mafunzo hayo yatawawezesha kutoa mafunzo ngazi ya jamii na kuleta tija kwa jamii.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 24,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.