MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma Menas Komba,amewakumbusha watumishi wa Halmashauri hiyo suala la uaminifu na uadilifu wanapopewa dhamana ya kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuepuka miradi kujengwa chini ya viwango.
Komba ametoa rai hiyo jana,wakati akizungumza na wananchi na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo wakati akabidhi eneo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mganga wa Hospitali ya wilaya katika kijiji cha Mpitimbi B wilayani Songea.
“hatuhitaji ubabaishaji katika mradi huu,tumepata shida sana kwenye baadhi ya miradi iliyotekelezwa uko nyuma,kuna mama mmoja alipewa kazi ya kusimamia miradi katika maeneo tofauti, sasa alichotufanyia hatuwezi kumsahau hata kidogo”.
Aidha,amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Neema Maghembe na wakuu wa idara kuhakikisha wanawapa kazi watu(mafundi) wenye uwezo ambao watafanya kazi kwa viwango kulingana na gharama halisi ya fedha zinazotolewa na Serikali.
“mkurugenzi sisi katika Halmashauri tuna mafunzi wazuri sana,waombe watatu au zaidi na washindanishwe ili apatikane mmoja mwenye uwezo kwa kufuata utaratibu na siyo kuteuliwa”alisisitiza Komba.
Komba,amewaasa wataalam wa Halmashauri hiyo kusimamia vizuri miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii na maisha ya wananchi na kuacha tabia ya kutanguliza maslahi binafsi kwa kuwa tabia hiyo inasababisha matumizi mabaya ya fedha za umma na kuwepo kwa miradi mibovu.
“msinunue vitu ambavyo viko chini ya viwango alafu vikatusumbua,pia mjiepushe kuongeze gharama ya bei kwenye manunuzi ya vifaa,tutakapogundua tutafuta hiyo kotesheni na kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtumishi aliyehusika”aliongeza.
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri,amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia mpango wa Tasaf kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kaya maskini hapa nchini na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama,kwa kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo ya Wananchi wa Jimbo hilo.
Alisema,nyumba hiyo itakwenda kupunguza tatizo la nyumba za watumishi na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwani nyumba hiyo itamwezesha Daktari kuishi jirani na eneo la kazi.
Komba ambaye ni Diwani wa kata ya Matimila,amewataka wasimamia wa mradi huo kuwa na daftari lenye orodha ya wanufaika wote watakao shiriki katika ujenzi wa nyumba hiyo ili siku ya malipo kusitokee malalamiko yasiokuwa ya lazima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Neema Maghembe alisema,shilingi milioni 68 zilizoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo zitatumika vizuri kama ilivyopangwa.
Alisema,Halmashauri kupitia wataalam wa idara imejipanga kuhakikisha miradi yote inayotekeleza na ile itakayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwamo ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa inakamilika kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Songea Pendo Daniel,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya umaskini kwa kutoa ruzuku ya fedha kwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini hapa nchini.
Amewataka wananchi wa kijiji hicho ambao ni walengwa wa mpango huo ,kujitokeza na kushiriki kwa karibu ujenzi wa nyumba hiyo ili waweze kujipatia kipato na ikamilike kwa muda uliopangwa.
Aidha,amewaagiza wasimamizi kutoa vifaa vya ujenzi kwa wakati ili mafundi waweze kutekeleza majukumu yao na kuweka maslahi ya Taifa mbele badala ya kutanguliza maslahi yao binafsi.
Awali Mtendaji wa kijiji cha Mpitimbi B Naomi Julius alisema,fedha zinazotarajiwa kutumika katika mradi huo ni Sh,milioni 68,376,000.0 zilizookolewa katika manunuzi ya vifaa vya miradi ya ajira za muda kwa mwaka 2021/2022.
Alisema, kwa kuwa fedha za kugharamia ujenzi wa nyumba ya Mganga zinatokana na utekelezaji wa miradi ya ajira za muda,ujenzi wa nyumba hiyo utafanywa na wana kaya wenye uwezo wa kufanya kazi toka kaya za walengwa wa kijiji hicho.
Alisema,muda wa utekelezaji wa mradi huo ni miezi sita na walengwa watafanya kazi kwa siku kumi kila mwezi na kila mlengwa atalipwa sh.3,00 kwa siku ili kuwawezesha kupata ruzuku au kipato cha ziada kwa ajili ya kujikimu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.