Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) linatarajia kufanya mkutano wake mkuu maalumu mnamo Aprili 5, 2025, mjini Songea, kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wapya wa jukwaa hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Hunt mjini Songea club,Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alisema Mgeni rasmi atakuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea mwenza wa urais wa mwaka 2025 kupitia chama hicho, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Balile alibainisha kuwa mwaliko wa Katibu Mkuu wa CCM ni sehemu ya utaratibu wa TEF wa kuwaalika viongozi wa vyama mbalimbali na serikali kwa lengo la kuonesha usawa na mshikamano.
Alitoa mfano wa mikutano iliyowahi kuwashirikisha viongozi kama Tundu Lissu na Freeman Mbowe, akisisitiza kuwa jukwaa hilo linajivunia kushirikiana na wanasiasa wa pande zote.
Katika mkutano huo, Balile aliwakumbusha waandishi wa habari kufuata miiko ya taaluma yao na kutokuegemea upande wowote wa kisiasa.
Aliwataka waandishi kuepuka kujiingiza katika kampeni za kisiasa au kuonesha upendeleo kwa chama chochote, badala yake kuwa waadilifu na wenye weledi.
Aidha, alikumbusha mchango wa TEF katika kukuza taaluma ya uandishi wa habari, akitaja mkutano mkubwa wa vyombo vya habari Afrika uliofanyika jijini Arusha mwaka 2022 na kuhudhuriwa na nchi 54.
Mikutano mingine ilifanyika Zambia mwaka 2023 na Accra, Ghana mwaka 2024, huku mkutano mwingine mkubwa ukitarajiwa kufanyika Morocco mwaka huu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.