KUNDI kubwa la Tembo wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 20, wamevamia katika makazi ya watu na mashamba katika kijiji cha Majimaji wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,na kufanya uharibifu na kula mazao mbalimbali.
Tembo hao wamesababisha hasara kwa wananchi wa kijiji hicho akiwemo Iman Kalembo,ambaye amepoteza mazao yake baada ya shamba lake lililokuwa na mapapai na miembe lenye ukubwa wa ekari 4 kuvamiwa na wanyama hao.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa Kalembo alisema,Tembo wamekula mapapai ambayo yalishaanza kukomaa na mengine kuanza kuiva,lakini ndoto zake za kujikwamua na umaskini kupitia kilimo zimeyeyuko kutokana na uvamizi uliofanywa na wanyama hao.
Kalembo,ameiomba Serikali kuchukua hatua za kudhibiti tembo hao wanaozurura ovyo kwenye makazi ya watu na mashambani na kula mazao,hali inayotishia kuwepo kwa upungufu mkubwa wa chakula katika kijiji hicho.
Msimamizi wa shamba hilo Ramadhan Kaundama alieleza kuwa,kundi la tembo lilianza kufika katika maeneo hayo saa 11 jioni lakini wananchi walifanikiwa kuwafukuza,hata hivyo usiku Tembo walirudi tena na kula mazao na kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu ya shamba hilo na mashamba ya wakulima wengine.
Aidha alisema,sasa wananchi wanashindwa kwenda mashambani kwa kuhofia kuvamiwa na tembo na baadhi yao wanalazimika kutoa mazao mashambani yakiwa hayajakomaa kwa kuhofia kuliwa.
Mkulima mwingine Sophia Imani amelalamikia uvamizi wa tembo kwenye mashamba na makazi yao,hali inayozidi kuhatarisha usalama wao na mali zao.
Alisema,licha ya kutoa taarifa kwenye mamlaka zinazohusika,lakini bado tembo wamezidi kuongezeka na kuendelea kuvamia kwenye shamba lake mara kwa mara.
Aliongeza kuwa, kuwepo kwa makundi ya tembo wanaofika hadi maeneo ya makazi yao usiku na mchana wanasababisha hata wanafunzi kushindwa kwenda shuleni na wengine kuchelewa vipindi vya asubuhi kwa kuhofia usalama wao.
Kwa upande wake Afisa Wanyama pori wilayani Tunduru Dauson Francis alisema,kimsingi wilaya ya Tunduru imeanzishwa na kuzungukwa katika maeneo ya mapito ya wanyama hasa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere zamani Selou.
Alisema,kuongezeko la matukio ya migogoro baina ya tembo na binadamu linachangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa shughuli kibinadamu katika maeneo ya mapito ya wanyamapori na yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi.
Alitaja changamoto nyingine ni ongezeko la watu na vijiji kutokuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi,hivyo kusababisha wananchi kupewa ardhi kwa ajili ya kulima na kufanya shughuli nyingine za kibinadamu kwenye mapito ya wanyamapori.
Alisema,chanzo kingine cha migogoro ni uingizwaji wa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa na hivyo kusababisha tembo kutoka hifadhini kwani baadhi ya mifugo huwa na harufu za dawa za kuzuia magonjwa jambo ambalo tembo hawapendi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.