WAKALA wa huduma za misitu Tanzania(TFS)wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,imetoa msaada ya vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati wa zahanati ya kijiji cha Misechela wilayani Tunduru.
Msaada uliotolewa na TFS ni mifuko 60 ya saruji,bati 10, misumari ya bati kilo 20,rangi ya mafuta lita 40 na rangi ya maji lita 80 vyote vikiwa na thamani ya Sh.milioni 2.
Akikabidhi msaada huo kwa serikali ya kijiji hicho,Mhifadhi wa misitu (TFS) Wilayani Tunduru Denis Mwangama alisema,wakala wa huduma za misitu Tanzania kwa kuendeleza ujirani mwema na ushirikkiano wa uhifadhi wa misitu inashiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi katika vijiji vinavyopakana na misitu za hifadhi.
Alisema,kijiji cha Misechela ni miongoni mwa vijiji 13 vinavyopakana na Hifadhi ya mazingira asilia Mwambesi yenye rasilimali nyingi ikiwamo wanyama aina mbalimbali,miti na mto maarufu wa Ruvuma unaopita katika wilaya zote tano za mkoa wa Ruvuma na baadhi ya wilaya za mkoa wa Mtwara.
Alieleza kuwa,kwa kutambua umuhimu wa afya ofisi ya wakala wa huduma za misitu Tanzania wilaya ya Tunduru inaungana na wananchi wa kijiji cha Misechela katika kazi ya ukarabati wa zahanati ya kijiji hicho kwa kutoa vifaa vya ujenzi kama mchango wake.
Alisema,TFS itaendelea kushiriki na kushirikiana na jamii katika kuboresha sekta ya afya kwa kuamini kuwa,jamii ya watu wenye afya njema wanamchango mkubwa katika kutunza rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha alisema,jamii na serikali za vijiji kila upande una wajibu wa kuhakikisha wanatunza misitu kwa kuwa,misitu ni sehemu ya chanzo kikubwa cha mapato inayoingizia Taifa fedha nyingi ambazo zinatumika kwa kuboresha na kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii hapa nchini.
Kwa upande wake Afisa mtendaji wa kijiji cha Misechela Daud Pendael, ameishukuru TFS kwa msaada huo na kuhaidi vifaa hivyo vitatumika kwa kazi iliyokusudiwa.
Alisema,kijiji cha Misechela ni miongoni mwa vijiji vyenye changamoto kubwa ya huduma za afya, hivyo wananchi wake wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda vijiji vingine kufuata huduma hizo.
Alisema,vifaa hivyo vinakwenda kuimarisha huduma za afya kwa kumaliza ukarabati wa zahanati ya kijiji hiyo ambayo kazi ya ukarabati ilisimama kwa kukosa vifaa vya viwandani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.