WAKALA wa huduma za misitu Tanzania(TFS)Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,imekabidhi mizinga ya nyuki kwa Serikali ya kijiji cha Mbati kwa ajili ya kuzuia wanyama waharibifu hususani Tembo wanaovamia mashamba na kula mazao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mizinga hiyo Meneja wa TFS Wilayani Tunduru Denis Mwangama alisema,ufugaji nyuki ni kati ya mbinu kubwa zinazotumika na kusaidia sana kuzuia Tembo kuingia kwenye makazi ya watu na mashambani.
Alisema utafiti uliofanyika umeonesha kuwa,ufugaji nyuki umeleta mafanikio makubwa katika maeneo yenye changamoto ya wanyama wakali na waharibifu wanaotoka porini au kwenye hifadhi na kwenda kwenye makazi ya watu na mashambani.
“kwa kawaida Tembo wanapopita kwenye njia zao na kugonga mizinga au miti ambayo imefungwa mizinga hiyo,na nyuki wakipata harufu ya wanyama hao wanatoka nje na kuwang’ata na hivyo kukimbia au kurudi wanakotoka”alisema Mwangama.
Mwangama alisema, mizinga hiyo ina thamani ya Sh.2,000,000/= na imefungwa kwenye maeneo yote ya mapito ya Tembo,kama mkakati wao wa kusaidia jamii kukabiliana na majanga mbalimbali.
Aidha alisema,TFS itaendelea kutoa mizinga kadri itakavyoweza ili kudhibiti vitendo vya uharibifu wa wanyama hao pamoja na kuhamasisha jamii kufuga nyuki kama sehemu ya kujiongezea kipato badala ya kutegemea shughuli moja tu ya kilimo.
Amewaomba wananchi wa kijiji hicho,kuhakikisha wanalinda mizinga hiyo na kuwa na utaratibu wa kukagua mara kwa mara ili kuifanyia usafi na matengenezo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kutimiza malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
Alisema,mizinga hiyo ni mali ya Serikali ya kijiji na sio ya mtu binafsi na ndiyo yenye mamlaka ya kutunza na kupanga matumizi yake kwa kuwashirikisha wana jamii(wananchi).
Kaimu Afisa Nyuki wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Micheal William,ameishukuru Wizara ya Maliasili na utalii kupitia wakala wa huduma za misitu nchini(TFS)kwa kuona umuhimu wa kutoa mizinga ya nyuki.
Alisema,mizinga hiyo itaongeza hamasa na kuongeza chachu ya ufugaji nyuki endelevu katika misitu ya asili na ile inayopandwa kama sehemu ya kipato cha mtu mmoja mmoja na jamii.
Michael alieleza kuwa,mizinga hiyo inakwenda kubadilisha ufugaji nyuki kutoka ule wa mazoea na kuwa wa kisasa na hivyo kuwaongezea kipato chao ambapo amewataka wananchi wa kijiji hicho, kulinda na kutunza mizinga hiyo ili iweze kusaidia kukabiliana na wanyama hao.
Amewaomba wadau wengine wa sekta ya misitu na nyuki nchini,kujitokeza na kuwasaidia wananchi wa Tunduru kukabiliana na wanyama waharibifu wa mazao ambao wamesababisha umaskini mkubwa kwa wananchi wanaotegemea shughuli za kilimo kuendesha maisha yao ya kila siku.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mbati Baslom Mkondya alisema, changamoto kubwa katika kijiji hicho ni Tembo ambao wanatoka kwenye hifadhi na kwenda kwenye mashamba ya wananchi na kula mazao.
Kwa mujibu wa Mkondya ni kwamba,hadi sasa jumla ya mashamba 115 sawa na ekari 500 za mazao mbalimbali zimeharibiwa na Tembo, jambo lililosababisha uchumi wa kijiji hicho kushuka na kutishia kuwepo kwa dalili za njaa na umaskini kwa baadhi ya kaya.
Alitaja mazao yaliyoshambuliwa na wanyama hao ni pamoja na Mbaazi,mpunga,mahindi,korosho na matunda mbalimbali yanayolimwa kwa ajili ya kuwaongezea kipato wananchi wa kijiji hicho.
Pia alisema kuwa,wanyama hao wanatishia usalama wananchi pindi wanapokwenda katika shughuli zao za uzalishaji mali na kuiomba serikali na wadau mbalimbali kujitokeza kudhibiti wanyama hao ili wasiendelee kuleta madhara makubwa kwa wananchi.
Mkazi wa kijiji hicho Mussa Abdala,ameishukuru TFS kupeleka mizinga hiyo kwa kuamini kwamba itasaidia sana kukabiliana na wanyama waharibifu ambao ni kero kubwa katika kijiji hicho.
Alisema,wanyama hao wamesababisha umaskini mkubwa kwa baadhi ya familia kwa kukosa chakula,kutokana na mazao yao kuliwa yakiwa bado mashambani na kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti wanyama hao wasiendelee kuleta madhara makubwa kwa jamii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.