Na Guspha Swai- RS Ruvuma
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetoa semina elekezi kwa wafanyabiashara,wajasirimali na wawekezaji wa Mkoa wa Ruvuma iliyofanyika Katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania tawi la Songea.
Semina hiyo imelenga kuwahamasisha wawekezaji kusajili biashara zao sambamba na kufahamu fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo ndani ya Mkoa wa Ruvuma na nchini kwa ujumla
Akizungumza kwenye ufunguzi wa semina hiyo,mgani rasmi katibu Tawala wa wilaya ya Songea Mtela Mwampamba ameishukuru TIC na Serikali kwa ujumla kwa juhudi za kuhakikisha inaandaa mazingira rafiki ya uwekezaji ndani ya Mkoa wa Ruvuma.
Amesema katika kuboresha miundombinu ya barabara mjini Songea kwa lengo la kuvutia wawekezaji,Manispaa ya Songea imepokea zaidi ya bilioni 22 za matengenezo ya barabara 22 kwa kiwango cha lami nzito.
Ameongeza kuwa pia serikali imetoa shilingi bilioni 19 za ujenzi wa masoko mawili ya kisasa mjini Songea pamoja na kuboresha sekta ya viwanda ikiwa ni juhudi za Serikali kuboresha shughuli za uwekezaji nchini
"Tumeshaletewa pesa zaidi ya bilioni 22 kuhakikisha ndani ya manispaa barabara zote zinakuwa za lami, lakini kwa kutambua kwamba watu wa Ruvuma ni wawekezaji wakubwa, tayari tumeshapokea shilingi bilioni 19 ili tuweze kujenga masoko mawili ya kisasa mjini Songea" Amebainisha
Naye Afisa Biashara Mkoa wa Ruvuma Joseph Martin Kabalo amezitaja fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana ndani ya Mkoa wa Ruvuma ikiwemo ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, fursa ya uuzaji wa bidhaa za viwandani, utalii, uvuvi na fursa ya usindikaji wa mazao mbalimbali hususani mahindi
Felix John ni Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka TIC amesema wapo Mkoani Ruvuma wakitekeleza kampeni ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani ambapo wametembelea miradi miwili ya wawekezaji wazawa wa ndani ya Mkoa wa Ruvuma.
Ameitaja miradi hiyo ni ya mwekezaji SUPERFEO aliyewekeza mradi wa kiwanda cha unga eneo la Namanditi mjini Songea na mradi wa uchimbaji wa makaa ya mawe unaofanywa na kampuni ya wazawa ya JITEGEMEE wilayani Mbinga.
Amesema TIC inatoa elimu endelevu ya uwekezaji na kuhamasisha usajili wa miradi ili wawekezaji waweze kunufaika na vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi vinavyotolewa na Serikali.
Kwa upande wake Rosemary Ngonyani ambaye ni Mfanyabiashara Mkoani Ruvuma ameishukuru Serikali kupitia kituo cha uwekezaji kwa kutoa semina hiyo ambapo amewahimiza wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma kukuza biashara zao na kuwekeza katika sekta mbalimbalimbali ili kuepuka kuwategemea wageni kuwekeza katika sekta hizo;
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Ndicho chombo cha msingi cha Serikali cha kuratibu, kuhimiza, kukuza na kuwezesha uwekezaji nchini Tanzania.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.