Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ruvuma imekabidhi rasmi gari aina ya ISUZU kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya matumizi ya serikali, baada ya kutaifishwa kutokana na kuingizwa nchini kinyume cha sheria.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Songea, ambapo Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma, Nicodemas Mwakilembe, alikabidhi gari hilo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilembe alieleza kuwa gari hilo awali liliingia nchini kwa kibali cha muda mnamo Januari 2024 likitokea Kenya, lakini lilirejea tena nchini mwezi Aprili 2024 bila kufuata taratibu za kisheria.
“Gari hili lilikutwa katika Kijiji cha Lusewa, Wilaya ya Namtumbo likifanya shughuli za kubeba mizigo kuelekea Masasi, Mtwara. Jeshi la Wananchi waliopo kijijini hapo waliliona na kulikamata. Baada ya uchunguzi wa kina, ilibainika kwamba gari hilo liliingia nchini kwa njia zisizo halali,” alisema Mwakilembe.
Aliongeza kuwa baada ya hatua zote za kisheria kufuatwa, TRA iliamua kutaifisha rasmi gari hilo na kulikabidhi kwa serikali kwa matumizi ya ofisi ya umma.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Bi. Mary Makondo, akipokea gari hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, aliishukuru TRA kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha rasilimali zilizotaifishwa zinatumika kwa manufaa ya wananchi.
“Tunashukuru kwa msaada huu wa gari ambalo litasaidia katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiutendaji katika Mkoa wa Ruvuma,” alisema Makondo.
Makabidhiano hayo ni sehemu ya jitihada za TRA za kuhakikisha sheria za kodi na forodha zinafuatwa kikamilifu, sambamba na kulinda maslahi ya taifa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.