Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma imefanikiwa kukusanya ufuta zaidi ya tani 2300 kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Ghala la Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) Sarah Chirwo wakati anatoa taarifa ya ununuzi wa ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu mjini Tunduru.
Amesema tani zilizonunuliw ni hadi kufikia Julai 16 mwaka huu na kwamba ukusanyaji wa ufuta bado unaendelea kwa kasi kubwa ambapo wakulima wanafurahia mfumo huo kwa sababu wanauza mazao yao kwa bei nzuri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru Musa Manjaule amesema wakulima wa Tunduru wameelewa faida za mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umemaliza kero ya muda mrefu ya kuibiwa kupitia mfumo holela wa kununua mazao.
“Sisi Tunduru ukituambia stakabadhi tuitoe hatuwezi kukuelewa,kwa sababu tunajua ubaya wa Mfumo holela wa kununua mazao”,alisema Musa.
Kwa upande wake Mkulima Rajabu Mohamed Mkazi wa Ligunga Tunduru amesema licha ya kujitokeza wakati fulani changamoto ya kuchelewa malipo,bado mfumo wa stakabadhi ghalani una faida nyingi kuliko hasara.
Akizungumza baada ya kusikiliza kero za wakulima Wilaya Tunduru,Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu ameahidi kushughulikia changamoto hizo ikiwemo ya kuchelewa kwa malipo na pembejeo za kilimo.
Katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani ameongozana na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania,Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma,Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mtendaji Mkuu toka Wakala wa Vipimo na Mwakilishi wa Kituo cha Utafiti wa Mazao TARI.
Mkurugenzi huyo anatembelea Wilaya zote ambazo zinanunua mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wakulima na kuzitafutia ufumbuzi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.