HOSPITALI ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na shirika la usimamizi na uboreshaji wa huduma za afya(MDH) imezindua mkakati wa kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutoa vifaa vya kukusanyia sampuli za makohozi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Mratibu wa MDH Dkt Nikson John alisema, vifaa hivyo vilivyotolewa kwa wahudumu wa afya ni kuunga mkono juhudi za Serikali na zinalenga kusaidia katika kampeni ya kutokomeza ugonjwa huo ambao bado umekuwa tatizo kwa jamii hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni.
Dkt Nikson alisema,MDH mkoa wa Ruvuma inasaidia eneo la kifua kikuu kwa kutoa vifaa na kuwawezesha wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu ambapo amevitaja vifaa hivyo ni wahudumu hao ni makoti ya mvua,buti, na vifaa vya kukusanyia sampuli za makohozi.
Alisema, vifaa hivyo vinakwenda kuongeza hamasa kwa wahudumu hao pamoja na kuleta tija katika kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu inayofanywa na Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma.
Kwa upande wake,Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole amewashukuru wadau Shirika la MDH kwa kutoa vifaa ambavyo vitasaidia katika kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu hasa wakati huu wa masika ambapo Jiografia ya wilaya hiyo sio rafiki kwa wahudumu hao ambao wanakwenda katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.
Alisema, vifaa hivyo vitawapa morali wahudumu hao kwa kufanya kazi katika mazingira yoyote bila kujali mvua au jua ambapo lengo la wilaya hiyo ni kufanya vizuri katika mapambano ya ugonjwa wa huo chini ya kauli mbiu kila unayemuona mbele yako ni “muhisiwa wa kifua kikuu”.
Alisema, vifaa hivyo vilivyotolewa katika kitengo cha kifua kikuu na ukoma vitaleta ufanisi mkubwa kwa kuibua wahisiwa wengi, kwani unapopata idadi kubwa ya wahisiwa ni dhahiri hata wagonjwa wataongezeka.
Dkt Kihongole alisema,lengo la wilaya hiyo ni kuendelea kuibua wagonjwa wengi ambao wataanzishiwa matibabu ili wilaya ya Tunduru ibaki salama bila maambukizi ya ugonjwa huo.
Naye muhudumu wa afya ngazi jamii Iddi Yakiti(Nyuki) amelishukuru Shirika la MDH kwa kutoa vifaa hivyo ambavyo vinakwnda kusaidia katika kazi ya kukusanya sampuli za makohozi vijijini na kuleta vituoni kwa ajili ya uchunguzi.
Alisema, awali utendaji wa majukumu yao ulikuwa mgumu kwani wakati mwingine walinyeshewa na mvua na kusababisha hata sampuli za makohozi nazo kulowa jambo lililosababisha kushindwa kufikia malengo yao.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.