UBORESHAJI wa kituo cha afya Mtakanini katika Halmasauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ,ambao serikali ilitoa sh.milioni 400 umefikia asilimia 95.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Dr.Godwin Luta akitoa taarifa ya kituo hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,amesema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa Ilani ya CCM wa kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya.
Amesema kiasi hicho cha fedha kimetumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje,maabara,choo cha wagonjwa wa nje,jengo la kufulia,chumba cha upasuaji na ukarabati wa jengo la mama na mtoto.
“Mradi huu utakapokamilika kwa asilimia 100,tutakuwa tumewapunguzia wananchi kero ya kusafiri umbali mrefu wa kutafuta huduma ya afya na upasuaji nje ya Halmashauri ya Namtumbo’’,alisisitiza.
Hata hivyo amesema hadi sasa zimetumika zaidi ya Sh.milioni 300 kutekeleza mradi huo na kwamba zimebaki shilingi milioni 95 kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo.
Akizungumza mara baada ya kukagua majengo ya kituo hicho,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewapongeza wananchi hao kwa kufikia hatua kubwa ya ujenzi unaotarajia kukamilika hivi karibuni.
Amesema serikali kwa wakati mmoja ilitoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vitatu mkoani Ruvuma, ambavyo ni Mgagagura,Mtakanini na Matimira.
Hata hivyo amesema vituo vingine bado havijaanza ujenzi wakati kituo cha afya Mtakanini kipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi.
Amesema ataviagiza vituo vingine ambavyo bado havijatekeleza mradi huo kufika kujifunza katika kituo cha afya Mtakanini kutokana na kufanya kazi nzuri ya ujenzi wa majengo sita na fedha imebaki.
“Kwa kuwa ujenzi unakwenda mwisho,nakuomba Mkurugenzi uanze mchakato wa manunuzi wa vifaa vya kituo hiki,vikiwemo vitanda, madogoro, mashuka,dawa na vifaa vingine vinavyotumika katika huduma ya afya’’,alisisitiza.
Mndeme pia amewaagiza RUWASA wilaya ya Namtumbo kupeleka maji katika kituo hicho, TANESCO kupeleka huduma ya umeme na TARURA kukamilisha matengenezo ya barabara haraka.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 12,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.