WAZIRI wa nishati Dkt Medard Kalemani, amezindua ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme vijijini(Rea) wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, na kutoa mwezi mmoja hadi tarehe 30 Agosti wakandarasi wa miradi hiyo kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa.
Amewataka wakandarasi wanaojenga mradi huo, kuhakikisha wanapeleka umeme katika vijiji vyote vilivyopangwa kufikiwa na mradi huo wa awamu ya tatu kwa kuwa wananchi wana hamu kubwa ili waweze kuutumia katika shughuli za uzalishaji.
Dkt Kalemani, ametoa agizo hilo jana wakati wa uzinduzi wa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili katika kijiji cha Nalasi wilaya ya Tunduru.
Dkt Kalemani amesema, suala la kuunganisha umeme hapa nchini sio hiari bali ni jambo la lazima,ndiyo maana Serikali imedhamiria kufikisha umeme katika vijiji vyote ambavyo vilisahaulika kwenye awamu mbili zilizopita katika wilaya hiyo.
Amewahidi wananchi na viongozi wa wilaya ya Tunduru kuwa,vijiji vyote vilivyobaki vinakwenda kupata umeme ndani ya mwezi mmoja kwa kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeshatoa fedha za kutekeleza mradi huo.
Amesema,mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili katika wilaya ya Tunduru umepangwa kufikishwa katika vijiji 85 na kuwasisitiza wakandarasi kutoruka hata kijiji kimoja wakati wa utekelezaji wa utekelezaji wake.
Dkt Kalemani amewaagiza viongozi wa shirika la umeme Tanesco wilaya ya Tunduru,kufungua ofisi ndogo katika kijiji cha Nalas ili wananchi wasiangaike kwenda hadi Tunduru mjini kwa ajili ya kulipia gharama za kuunganishiwa umeme kwenye makazi yao.
Aidha, amewakumbusha viongozi wa Serikali za vijiji kutenga maeneo maalum ya uwezekaji ili yaweze kupelekewa miundombinu ya umeme wakati wa utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini.
“nawaomba sana viongozi wa serikali za vijiji kutenga maeneo ya uwekezaji ili yapelekewa umeme na tumieni umeme utakaoletwa kufanya biashara na kuongeza thamani ya mazao yenu ya kilimo na mifugo na kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa”amesema Dkt Kalemani.
Amesema, miradi ya kusambaza umeme katika vijiji vilivyosahaulika ndani ya mkoa wa Ruvuma utatekelezwa kwa muda wa miezi 18 na Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 71na unatekelezwa na wakandarasi watatu ili kuharakisha utekelezaji wake.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge ameishukuru Serikali kupitia wizara ya nishati kuanza ujenzi wa mradi huo ambao unakwenda kuharakisha uchumi wa mkoa wa Ruvuma.
Aidha, amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaohujumu na kuiba miundombinu ya umeme na kuwataka kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
“tunaleta umeme wana Nalasi, maeneo mengine ambako umeme unapita wameanza kujisahau wanaiba nyaya,yaani juhudi na fedha zote zaidi ya bilioni 71.1 zimeletwa kwa ajili ya Ruvuma pekee yake ikiwemo hapa Nalasi, lakini kichaa mwingine kwa maslahi yake anajiamulia kwa kuiba nyaya za umeme,tabia hiyo inarudisha nyuma juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo”amesema Jenerali Ibuge.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini Daimu Mpakate amesema, jimbo la Tunduru kusini lina vijiji 65 lakini vilivyofikiwa na umeme ni 12 tu ambapo ameiomba wizara ya nishati kukamilisha kazi hiyo haraka ili wananchi watumie umeme huo kujiletea maendeleo.
Imeandikwa na Muhidin Amri,Tunduru
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.