Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amezindua kampeni ya upandaji wa miti katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambayo imefanyika katika shamba la kampuni ya Aviv Tanzania Limited inayojishushulisha na kilimo cha kahawa mkoani Ruvuma.
Kampeni hiyo iliyoandaliwa na kampuni ya Aviv kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kutunza mazingira imezinduliwa kwa kupanda miti pembezoni mwa milima ya Litenga katika shamba la kahawa la Aviv lililopo Lipokela Wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Kabla ya uzinduzi huo Kanali Ahmed, amewasisitiza wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti na kuitunza ili iweze kukua na kuona matokeo ya upandaji huo, pia ameipongeza Aviv Tanzania Limited kwa kuzingatia sheria za nchi na kimataifa kwa kupanda miti.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mary Makondo, amesema wataendelea kushirikiana ili zoezi hilo liwe endelevu kwa kuhimizana kupanda miti mingi na kuitunza ili kuhakikisha mazingira yanaendelea kuboreshwa na isaidie kuleta mvua nyingi zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, amebainisha kuwa Aviv imetoa miche laki moja kwaajili ya kupanda katika mashamba ya kahawa, pia amewasisitiza wakulima wa kahawa kutokata miti ya asili ili kupanda kahawa badala yake wanatakiwa kupanda miti mingine ili kutunza mazingira na kupata soko la zao hilo kutokana na sera za kimataifa.
Kwa upande mwingine Meneja wa Aviv Tanzania Limited, Hamza Kassim, amesema Aviv ipo pamoja na Serikali na sera ya Umoja wa Mtaifa katika kuhakikisha suala la mazingira linakuwa namba moja kwa kuwaelimisha wananchi maana ya uhifadhi wa mazingira ili nchi isigeuke jangwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.