Waziri wa Afya, Mheshimiwa Jenista Mhagama, amezindua usambazaji wa ripoti ya utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI kwa mwaka 2022/23 mkoani Ruvuma.
Uzinduzi huo umefanyika katika Kongamano la Kitaifa la Kisayansi lililofanyika katika ukumbi wa Chandamali mjini Songea, ikiwa ni sehemu ya matukio muhimu kuelekea maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, Disemba Mosi, ambayo yatafanyika mkoani hapo.
Katika uzinduzi huo Mhe. Jenista amesisitiza kuongeza bidii katika kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
"Kiwango cha ushamari wa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kimepungua kitaifa kutoka 7% mwaka 2003/2004 mpaka 4.4% mwaka 2022/23, jambo lingine ambalo tunatakiwa kujipongeza lakini tunatakiwa kuongeza bidii ni kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambacho nacho kimepungungua kutoa 18% mwaka 2010 hadi 8.1% mwaka 2023.
Amehimiza kila mmoja kulinda mafanikio yaliyopatikana na kuhakikisha Taifa linafanya vizuri zaidi katika mapambano dhidi ya UKIMWI, na amewataka TACAIDS kuendelea kuweka utaratibu wa kusikiliza na kutatua malalamiko yanayotokana na unyanyapaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), John Kamwela amesema utafiti huo uliofanyika ni hatua muhimu katika kutoa taswira halisi ya nchi katika kufikia malengo ya kimataifa ya kumaliza janga la UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Amesema majibu ya utafiti huo yatasambazwa katika ngazi za mikoa na wilaya ili kuwezesha watu wa maeneo hayo kupata taarifa za utafiti na kuboresha utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika maeneo hayo.
Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, Salum Kasssim Ali, akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Tanzania Dkt. Albina Chuwa amesema takwimu rasmi zilizotokana na utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI kwa mwaka 2022/23 zitatumika kupanga dhima na kutekeleza mipango ya kitaifa na kimataifa na kufuatilia programu mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Utafiti huo umesimamiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Zanzibar (ZAC), ukiratibiwa na Ofisi za Takwimu Tanzania (NBS) na Zanzibar (OCGHS), na kufadhiliwa na PEPFAR na kupata msaada wa kiufundi kutoka CDC na Shirika la ICAP la Chuo Kikuu cha Columbia, Marekani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.