Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma (MBIFACU) kimefanikisha ukusanyaji wa zao la kahawa kavu hadi kufikia zaidi ya tani 20,000 katika msimu wa mwaka 2021/2022.
Akizungumza wakati anatoa taarifa ya MBIFACU kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu,Kaimu Meneja wa MBIFACU Henerick Ndimbo amesema katika msimu wa mwaka 2021/2022 bei ya kahawa katika vyama vyote vya msingi imepanda hadi kufikia zaidi ya shilingi 7,000/= kwa kilo.
Amesisitiza kuwa Mfumo wa stakabadhi ghalani umeleta faida nyingi kwa mkulima ikiwemo kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo na kwamba katika kipindi cha miaka mitatu ushirika katika Wilaya ya Mbinga unaendelea kuimarika.
Faida nyingine ambazo wakulima wamezipata kupitia mfumo huo amezitaja kuwa ni kupunguza mfumo wa kilanguzi,kuanzishwa minada ya kikanda ya kahawa na wanachama kwenye vyama vya Msingi kupata Bima ya afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu amekipongeza Chama kikuu cha Ushirika Mbinga kwa kuimarisha Ushirika.
"Lengo la ziara yetu ni kukutana na wakulima ili kujionea wenyewe changamoto na mafanikio katika utekelezaji wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nichukue fursa hii kuwapongeza Mbinga mnafanya kazi nzuri inayoheshimika ",alisema Bangu.
Ameahidi kutafutia ufumbuzi changamoto zinazotokana na utekelezaji Mfumo wa stakabadhi ghalani ikiwemo ya kuchelewa kwa malipo na upungufu wa pembejeo za kilimo ambazo hazikidhi mahitaji ya wakulima.
Akizungumza na wakulima wa kahawa katika Chama cha Msingi Mahenge Mbinga Mkurugenzi huyo wa stakabadhi ghalani amewapongeza wananchi hao kwa kuanzisha miradi mbalimbali iliyotokana na mfumo wa stakabadhi ghalani ikiwemo kuanzisha Shule ya sekondari na miradi ya utengenezaji sabuni na batiki.
Naye Afisa Kilimo Mkoa wa Ruvuma Onesmo Ngao Akizungumza na wakulima wa Chama cha Msingi Mahenge ameagiza kila chama cha Msingi cha Ushirika kuanzisha kitalu chake cha miche ya kisasa ya kahawa.
Amesema uzalishaji wa miche ya kahawa utawezesha kufikia lengo la la kitaifa la kuzalisha tani laki tatu za kahawa.
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo inatekeleza kwa mafanikio makubwa mfumo wa stakabadhghalani ambao unamlinda mkulima dhidi ya walanguzi wa mazao ya kahawa,ufuta,soya,mbaazi na korosho.
imeandikwa na Albano Midelo
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.