KUELEKEA Tamasha la Kitaifa la Utamaduni, linaloanza kati ya Septemba 20 hadi 23 mwaka huu, kuna makubwa ya kisakolojia katika maisha ya umma huo, hasa wakazi wa kijiji cha Mbingamharule wilayani Songea, mkoa wa Ruvuma.
Hapo hija inateka saikolojia na fikra zao, wakiwa na mitazamo chanya nayo, ikiwamo kinachotambuliwa kama “kaburi lenye maajabu la kiongozi kimila, Chifu Ngosi Mharule bin Zulu Gama.”
Agnes Ngonyani, Msimamizi wa Kaburi hilo la kihistoria, ambalo sasa limejengwa umbo la duara kwenye eneo la ekari nne, ni moja ya vitu sasa vinapata hadhi ya kitalii, kijijini hapo.
Chifu Mharule, alitokea nchini Afrika Kusini na kwenda kutawala katika kabila hilo la Wangoni kuanzia mwaka 1847 hadi 1889 alipofariki na kuzikwa kijijini hapo.
Historia inaonyesha kuwa baada ya kufariki Chifu Mharule, alizikwa kwa kufuata desturi na mila za kichifu za kabila la Wangoni toka Afrika Kusini na wakati anazikwa, walichukuliwa watu wengine wawili hai na kuzikwa naye kwenye kaburi moja.
“Chifu Mharule baada ya kufariki mwaka 1889, alizikwa kwa taratibu za jadi ya machifu wa Afrika Kusini, kaburi lake lilikuwa la mviringo, sanda yake ilikuwa ya ngozi.
“Alikalishwa, kwenye kiti cha ngozi na walichukuliwa na watu wengine wawili wakiwa hai, ambao walizikwa pamoja naye kwenye kaburi moja wakiwa wamesimama mbele na nyuma ya mwili wa Chifu,” anasimulia Ngonyani.
Anasema kwa historia ya mila na desturi ya Kingoni, taratibu za kijadi za wakati huo zilitaka mfalme au chifu anapofariki, lazima azikwe na watu wawili wakiwa hai na kwamba hiyo ilikuwa ni amri ya serikali ya jadi na hapakuwapo anayepinga.
Kwa mujibu wa Mzee Ngonyani, wengi waliozikwa na Mfalme, ni wale waliozoeana na kufanya kazi kwa karibu.
Mbali na shughuli za utalii, kaburi hilo limekuwa likitumiwa na wananchi kwenda kuhiji kila mwaka na hata ndugu wa Chifu Mharule kutoka Afrika Kusini, huafika kufanya matambiko kwenye kaburi hilo.
"Mwaka 2019 ukoo wa Chifu Mharule kutoka Afrika Kusini ulifika kushuhudia kusimikwa kwa Chifu Nkosi Imanuel Zulu Gama wa Tano, ambaye ndiye Chifu wa Wangoni kwa sasa. Kwa hiyo yeyote anayependa kwenda kutembelea kaburi hilo.
VYA KUSHANGAZA
“Kuna taratibu zake za kimila, ambazo zinatakiwa kufuatwa ambazo ni kubeba mahindi na ulezi ambao unatengenezwa na bibi katika kijiji hicho.
"Baada ya kufika eneo la kaburi, anatangulia mhusika ambaye anawasiliana na Chifu kwa lugha ya jadi, ndipo waliofika kutambika wanaitwa na kupiga magoti juu ya kaburi na kuomboleza kwa sala za jadi.
“Baada ya maombi kuku au mbuzi wanachinjwa juu ya kaburi la Chifu Mharule, lakini jambo la kushangaza mbuzi huyo anapochinjwa hapigi kelele na baada ya kuchinjwa mmoja wa watambikaji anamwaga unga wote juu ya kaburi,” anasimulia Ngonyani.
Anataja lingine analoliita la kushangaza, mtu anapoenda hapo siku inayofuata kwenye kaburi, haoni damu wala unga, ikiwa ishara wanayoamini “kukubaliwa shida zote’ ambazo mtambikaji alikwenda nazo kuomba kwenye kaburi hilo.
Agness, ambaye amepewa kazi ya kusimamia kaburi hilo kwa sasa, anasema wamekuwa wakipokea wageni wengi wanaotembelea kaburi hilo na kwamba wapo ambao wanatoka mpaka nchi za Ulaya, Marekani na Afrika ambao nao huenda kuomba kutatuliwa shida zao mbalimbali, kuhiji na kufanya matambiko.
Agness anasema, maajabu mengine yaliyopo katika kaburi hilo ni pamoja na kuwapo kwa nyoka ambaye huonekana baada ya miaka mitano au kumi ambaye hata hivyo anapojitokeza kwa kipindi hicho ni watu watu ambao hubahatika kumuona.
“Huyu nyoka haonekani mara kwa mara, isipokuwa baada ya miaka mitano au kumi tena akijitokeza, watu wachache sana ndio hubahatika kumuona na akionekana huwa anaenda bondeni kunywa maji,” anasema Agness.
Anasimulia kwamba, eneo hilo la kaburi linaheshimika na hakuna mtu mwenye uthubutu wa kufanya uharibifu wowote.
“Kwa mfano, kwenye kaburi hilo la Chifu Mharule, kuna mtu aliwahi kwenda akaezua paa lakini hakuchukua hata mwezi mmoja alifariki, kwa hiyo tunaamini kwamba sababu hiyo ndio ilisababisha kifo chake,” anasema Agnes.
Anataka kwamba eneo hilo la kaburi la Chifu Mharule lenye heka nane linahitaji kuendelezwa na kulindwa, ili maajabu yaliyopo hapo yaendelee kuvutia watalii.
"Eneo lenye nafasi kama hili na lenye historia kubwa linahitaji kulindwa na kuendelezwa ili yale yaliyopo hapa yasipotee, kwa hiyo tunakaribisha wawekezaji, waje wawekeze na kutuinulia mila na desturi zetu zilizoasisiwa na wazee wetu,” anasema Agnes.
Septemba 20 mpaka 23 mwaka huu linafanyika Tamasha la Kitaifa la Utamaduni na miongoni mwa vivutio vya utalii wa kitamaduni vinavyobeba idadi kubwa ya watalii hususani katika kipindi hiki linapofanyika tamasha hilo ni wengi wao kushuhudia kaburi hilo la maajabu.
Rais Samia Suluhu Hassan, ndiye anatarajiwa kufunga tamasha hilo siku ya kilele chake Septemba 23 mwaka huu, hivyo mwangalizi wa kaburi la Chifu Mharule anasema ujio wake mkoani Ruvuma huenda ukaongeza idadi kubwa ya watalii wanaotembelea eneo hilo la kaburi.
"Ujio wa Tamasha la Kitaifa la Utamaduni kwenye mkoa wetu, kwetu ni fursa ya kutuongezea watalii kwenye vivutio vyetu, na hata ujio wa kiongozi mkubwa kama Rais unasaidia kutuletea watu wengine wengi, kwa hiyo tunawaalika waje kutembelea na kujionea maajabu yaliyopo kwenye kaburi hili la Chifu Mharule,"anasema Agnes.
"Tunanaamini kwamba Rais Samia (Samia Suluhu Hassan naye akija kufanya utalii hapa kwetu, ataguswa na vivutio hivi vya utalii wa kiutamaduni na kuviendeleza," anasema.
Hadi sasa mkoa wa Ruvuma, umo katika maendeleo yenye vivutio vingi vya utamaduni na ndipo hata serikali ikaelekeza Tamasha la Kitaifa la Utamaduni, kuenzi mambo yanayofanana na hayo.
Kaburi la chifu wa wangoni
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.