MSAJIRI wa Jumuiya za Kiraia kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Imanuel Kihampa amewatahadharisha viongozi wa dini kujiepusha na utakatishaji wa fedha haramu na kufadhili vitendo vya ugaidi.
Kihampa ametoa tahadhari hiyo wakati anatoa semina ya viongozi wa dini wa Mkoa wa Ruvuma iliyofanyika kwenye ukumbi wa sekondari ya Songea Girls mjini Songea.
“Kwa bahati mbaya baadhi ya viongozi wa dini nchini wameruhusu Taasisi zao kutumika kutakatisha fedha haramu ambapo wameruhusu fedha chafu na kuziingiza kwenye mzunguko halali wa kifedha za kibenki ili ionekane ni fedha halali’’,alisema.
Amesema kwa kutokujua au makusudi baadhi ya viongozi wa dini wametengeneza mianya ya Taasisi zao kuruhusu utakatishaji wa fedha haramu kufanyika na kwamba serikali ilikuwa haiwatilii mashaka viongozi wa dini kwa sababu serikali ina Imani kubwa na viongozi wa dini.
Amesisitiza kuwa viongozi wa dini ni wadau muhimu katika maendeleo ambapo amesikitishwa na baadhi ya viongozi wa dini kuruhusu vitendo hivyo kufanyika kupitia Taasisi zao ambapo amesema vitendo hivyo vina waweka viongozi wa dini kwenye mazingira ambayo sio salama yatakayowaingiza kwenye mtego mbaya na kuliingiza Taifa kwenye matatizo .
Amesema watu wenye nia ovu wanawaona viongozi wa dini kama mawindo hivyo wanaweza kuwatumia kufanikisha malengo maovu kwa kutumia mianya iliyopo kwenye Taasisi za dini ikiwemo utakatishaji wa fedha haramu na kufadhili ugaidi.
Awali akizungumza wakati anafungua semina hiyo,Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Joel Mbewa amesema serikali inatambua mchango wa Taasisi za dini katika kudumisha amani na utulivu nchini na kutoa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo huduma za elimu na afya.
Amesema serikali itaendelea kukuza ushirikiano na Taasisi za dini ili kuhakikisha kuwa jumuiya za kidini zinajiendesha kwa uhuru na kwa kuzingatia sheria,mila na desturi.
Hata hivyo Katibu Tawala huyo ametahadharisha kuwa nchini yetu imekumbwa na viashiria vya uvunjifu wa maadili ya kijamii na jumuiya nyingi kuonekana kuwa katika hatari ya kuweza kutumika katika kuwezesha makosa ya utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.
Mbewa amewaeleza viongozi hao,mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kutambua namna ya kuendesha jumuiya zao kwa kuzingatia sheria hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kulinda raslimali za jumuiya na kutojiingiza katika makosa ya utakatishaji wa fedha haramu,ufadhili wa ugaidi na biashara haramu za silaha za maangamizi.
Kwa upande wake Shehe wa Mkoa wa Ruvuma Ramadhani Mwakilima ameishukuru Ofisi ya Msajiri wa Jumuiya za Kiraia kwa semina hiyo ambayo imewaongezea maarifa na kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuendesha Taasisi za kidini.
Naye Mwakilishi wa Kanisa Katoliki Sr.Janeth Hyera amesema semina hiyo imewakumbusha mambo mbalimbali yaliyopo kwenye Taasisi wanazozisimamia ambayo yamesababisha baadhi ya Taasisi za kidini kufungiwa kwa kutotekeleza sheria na miongozo ya serikali.
Amesisitiza kuwa hivi sasa mambo mengi yanayofanyika inawezekana baadhi ya viongozi wa dini wanachangia kuwepo kwa maovu hayo ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu ambao unapoteza vijana wengi ambao wanadai wanapata fursa ya Kwenda kusoma nje ya nchi ambako wanatendewa mambo mengi ya kigaidi.
Naye Katibu wa Kamati ya Amani Mkoa wa Ruvuma Askofu Elimu Mwenzegule amesema mafunzo yamewashirikisha viongozi wa dini kutoka wilaya zote mkoani Ruvuma ambapo ameishauri serikali kuhakikisha semina muhimu kama hizo ziwe endelevu ili kuwajengea uwezo viongozi wa dini ambao wanawajibu mkubwa wa kudumisha amani na utulivu hapa nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.