MKUU Wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Mheshimiwa Pololet Mgema ameitaja vita kubwa na mbaya ambayo inakuja ni ya kugombania maji.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea,Mgema amesisitiza kuwa vita hiyo itasababishwa na uharibufu wa vyanzo vya maji unaoendelea hivi sasa.”Tutakapoharibu vyanzo vya maji kila mahali,kutakuwa na maeneo machache ambayo yatakuwa na maji,kila mtu atakwenda kwenye maeneo hayo kwa sababu maji ni uhai na ndipo tutakapopambana na kuuana kwa kugombea maji “,alisisitiza Mgema.
Hata hivyo ametahadharisha kuwa ili Dunia isifike huko shughuli zote za kibinadamu zisifanyike kwenye vyanzo vya maji.
Amewaagiza mameja wa maji Bonde la Mto Ruvuma na Ziwa Nyasa,kushirikiana na Jumuiya za watumia maji na maafisa Mazingira kusimamia vyanzo vya maji ili visiharibiwe.
Kwa upande wake Meneja RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles akizungumza kwenye mkutano huo amewaasa wananchi kulinda na kutunza vyanzo vya maji ili viwe endelevu.
Amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetenga bajeti kubwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji hivyo ni muhimu kulinda vyanzo vya maji ili miradi ya maji iwe endelevu.
Sheria ya raslimali za maji namba 11 ya mwaka 2009 imeagiza kulinda na kuhakikisha vyanzo vya maji haviharibiwi .
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Desemba 11,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.