WACHIMBAJI wadogo wa dhahabu wanaofanya shughuli zao katika kijiji cha Lukalasi kata ya Kigonsera wilayani Mbinga,wameiomba Serikali kuwasogezea Huduma za Afya kwa kujenga zahanati au kituo cha Afya ili waweze kupata huduma za matibabu ikiwemo za kifua kikuu na chanjo ya Covid-19.
Wametoa maombi hayo jana, wakati wa zoezi la kampeni ya uibuaji na upimaji wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu(TB) kwenye machimbo inayofanywa na Hospitali ya Halmashauri ya wilaya Mbinga na wataalam wa shirika la Management and Development for Heath(MDH).
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji hao Elimwaria Muro alisema, katika eneo hilo kuna watu zaidi ya elfu mbili wanaofanya kazi ya kutafuta na kuchimba dhahabu lakini hakuna huduma za afya.
Hivyo alisema, wakati umefika kwa Serikali kupitia wizara ya afya kuwajengea zahanati au kituo cha afya ili jamii inayoishi eneo hilo waweze kupata huduma za matibabu jirani na makazi yao.
Kwa mujibu wa Muro,iwapo Serikali itasogeza huduma za afya katika eneo hilo jamii itakuwa na afya njema na kuwawezesha kushiriki kazi mbalimbali za maendeleo na kutoa mchango mkubwa kujenga uchumi wa nchi yao.
Aidha Muro ambaye ni Mhandisi wa mgodi wa dhahabu wa Lukalasi unaomilikiwa na mzawa Jonson Nchimbi, ameipongeza Serikali kupitia wizara ya afya kupeleka huduma ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutumia cliniki inayotembea(Mobile Clinic) kwa wananchi waishio maeneo ya machimbo ya madini.
Edwin Nchimbi alisema, kwa sasa wanalazimika kutembea umbali mrefu hadi kijiji cha Kigonsera au Mbinga mjini kufuata matibabu,jambo ambalo ni kero kubwa na linawapotezea muda mwingi wa kufanya kazi za maendeleo.
Naye Dkt Bingwa wa magonjwa ya ndani ya Binadamu Dkt Dennis Ngatenelela alisema,serikali imelazimika kutumia cliniki inayotembea kuwafikia wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni ili waweze kupata huduma mbalimbali za afya.
Alisema, mpango wa Serikali kupitia wizara ya afya ni kuhakikisha kila mtu anapata huduma pale alipo na hakuna mwananchi atakayepoteza maisha kwa kukosa matibabu,ndiyo maana wamelazimika kupeleka huduma za uchunguzi hadi katika maeneo hayo.
Akizungumzia ugonjwa wa kifua kikuu Dkt Dennis alisema, tafiti za kitaalam zinaonesha kuwa kuna uhusiano wa karibu kati ya shughuli za uchimbaji wa madini na ugonjwa wa kifua kikuu kutokana na vumbi linalotoka wakati wa kutafuta na kuchimba madini kuingia ndani ya mwili wa Binadamu.
Alisema,wadudu wa kifua kikuu mara nyingi wanakaa katika miili ya binadamu na ugonjwa huo unatibika kwa mtu aliyeambukizwa kupata matibabu yanatolewa bure katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Dkt Bryson Mapunda alisema, matibabu ya kifua kikuu ni ya miezi sita na mgonjwa anatakiwa kunywa dawa kila siku bila kuacha.
Alisema, ni muhimu kumaliza dozi au matibabu kama ilivyoelekezwa na muhudumu wa afya na kuonya kuwa, kuacha kunywa dawa kikamilifu kuna weza kusababisha vimelea kuwa sugu na hivyo kuambukiza watu wengine.
Dkt Mapunda alisema, kifua kikuu sio ugonjwa wa kulogwa wala kurithi bali ni ugonjwa unaoambukizwa na vimelea aina ya bakteria visivyoonekana kwa macho bali kwa kutumia hadubini.
Amewashauri, watu wenye dalili za ugonjwa huo kuwahi kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na kifua kikuu kinatibika na kupona kabisa hata kama ana mgonjwa maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Alisema, mtu anapaswa kupata matibabu mapema ili kuzuia maambukizi kwa wengine na mgonjwa ambaye ameanza tiba sio rahisi kuambukiza mtu mwingine,hivyo hakuna sababu ya kumtenga.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.