Na Albano Midelo,Songea
WAFANYAKAZI 56 wa vituo vya kulelea Watoto wadogo mchana wilayani Songea mkoani Ruvuma wameanza mafunzo ya siku tano kwenye ukumbi wa Anglikana mjini Songea.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI na kusimamiwa na Idara ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma ambapo wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Taasisi ya ANJITA ambayo imepewa Mamlaka ya kutoa mafunzo hayo.
Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo,Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma Victor Nyenza amesema katika Mkoa wa Ruvuma kuna vituo 138 vya kulelea Watoto wadogo mchana na kwamba kati ya vituo hivyo ni vituo 68 tu ndiyo vimesajiriwa.
Ametoa rai kwa vituo ambavyo bado havijasajiriwa kuhakikisha wanavisajiri vituo vyao na kwamba ifikapo Januari 2024 vituo vyote viwe vimesajiriwa vinginevyo vitafungwa.
“Hatutarajii katika Mkoa wa Ruvuma kuwa na kituo cha kulelea Watoto mchana ambacho hakisajiriwa na kina walezi wa Watoto wasiokuwa na sifa ya mafunzo elekezi kwa vitendo,vituo ambavyo vitakuwa havina sifa tutakwenda kuvifunga kwa mujibu wa sheria’’,alisisitiza Nyenza.
Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa walezi wa watoto kwa kuwa wanakwenda kupata mbinu na stadi mbalimbali za kuboresha na kuimarisha malezi ya Watoto wanaohudumiwa.
Amesisitiza kuwa vitendo vingi vya ukatili wa Watoto na matukio mengi ya utekaji na utelekezaji wa Watoto yanafanyika pia kwenye vituo vya kulelea Watoto wadogo na kwamba Watoto wengi wanatekwa wakiwa katikati ya kituo cha malezi na nyumbani hivyo ameagiza kila kituo kiwe na rejesta ili kusaidia wamiliki wa vituo kujiweka upande salama.
Amelitaja jukumu la walezi wa Watoto wadogo mchana kuwa ni kumwandalia mazingira wezeshi mtoto ili aweze kukua vizuri na kuelewa stadi tatu za kusoma,kuandika na kuhesabu.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo Mratibu wa mafunzo kutoka Taasisi ya ANJITA Janeth Malela amezitaja mada ambazo zitafundishwa kwenye mafunzo hayo kuwa ni sayansi ya dhana ya malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto uanzishaji na usimamizi wa vituo vya Watoto na vifaa vya kujifunzia na kuchezea Watoto.
Mada nyingine amezitaja kuwa ni mbinu za ujifunzaji na kuelewa Watoto kuanzia miezi sita hadi miaka sita,afya lishe na usafi wa mazingira,ulinzi na usalama kwa mtoto,utambuzi wa mapema na afua stahiki kwa Watoto wenye mahitaji maalum,namna ya kufanya tathmini ya maendeleo ya mtoto na mafunzo kwa vitendo.
Aliyesimama ni Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma Victor Nyenza akizungumza wakati anafungua mafunzo ya wanafanyakazi wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana kwenye ukumbi wa Kanisa Anglikana mjini Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.