WAFUGAJI Songea washauriwa kutumia teknolojia rahisi ya ufugaji kuku
Wafugaji wa kuku wa Kijiji cha Nakahegwa wilayani Songea mkoani Ruvuma wameshauriwa kutumia teknolojia rahisi katika kufanikisha malengo yao ya ufugaji ili waweze kupata mafanikio ambayo yatawawezesha kupunguza umasikini wa kipato katika kaya zao.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Dr Erick Kahise katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wafugaji kuku wa kikundi cha Federation Moja kilichopo katika kijiji hicho.
Dr Kahise amesema ili mfugaji wa kuku aweze kupata mafanikio chanya afuate kanuni na taratibu za ufugaji kupitia teknolojia rahisi ikiwemo ujenzi wa mabanda ya kawaida ambayo vifaa vyake vinapatikana katika mazingira wanayoishi.
Amewashauri wafugaji kuwashirikisha wataalam wa mifugo kuanzia hatua ya awali ya utayarishaji wa banda, matumizi ya chanjo na utengezaji wa chakula ambao unafaa kulisha kuku.
“Ufugaji usiozingatia kanuni na taratibu za ufugaji unasababisha hasara kwa wafugaji kufuatia kuku hasa vifaranga kukumbwa na magonjwa na vifo jambo linalorudisha nyuma jitihada za kujinasua na umaskini wa mtu mmoja mmoja au kaya’’,alisisitiza Dr.Kahse.
Kwa upande wake Mlezi wa kikundi hicho Remigiusi Mbawala amesema kikundi hicho ni cha hiari ambacho kinamtaka kila mwanachama kutekeleza majukumu yake bila shuruti ili aweze kujipatia kipato chake kupitia mradi wa ufugaji kuku.
Naye Mratibu wa kikundi hicho Sponsa Dimayo amewaomba wataalam wa mifugo mara kwa mara kuwatembelea na kuwapa elimu na ushauri ambao utawabadilisha kimtazamo kuacha kufuga kuku kwa mazoea na kuanza kufuga kuku kwa njia ya kisasa.
Mratibu Mfuko wa Wanawake kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Songea Xveria Mlimira amewataka wanakikundi kutimiza vigezo vya kukopeshwa ili waweze kukopeshwa mikopo inayotolewa na Halmashauri hali itakayosababisha ufugaji kuwa endelevu.
Kikundi cha Fideration Moja kilianzishwa mwaka 2016 kikiwa na jumla ya kina wanachama 12 ambao wanajishugurisha na shughuri ya ufugaji kuku na kilimo cha mazao ya bustani.
Imeandikwa na Albano Midelo
Desemba 10,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.