WAZIRI wa maliasili na utalii Dkt Damas Ndumbaro, ametangaza
operesheni kabambe ya kuwaondoa wafugaji wote waliovamia na kufanya
shughuli zao katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere na maeneo mbalimbali
yaliyotengwa kwa ajili ya utalii hapa nchini.
Dkt Ndumbaro ametangaza hatua hiyo jana wakati akiongea na wananchi wa
vijiji vya Kalulu na Jakika wilayani Tunduru, wakati wa ziara yake ya
kusikiliza kero ya wananchi kuhusiana na wanyamapori wanaovamia
mashamba na kufanya uharibifu wa mazao wilayani humo.
Alisema, tatizo la wanyama hususani Tembo wanaokula mazao ya wakulima
limechangiwa kwa kiasi kikubwa na wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye
maeneo yasioruhusiwa kisheria jambo linalosababisha wanyama hao
kukimbia.
Kwa mujibu wa Dkt Ndumbaro Serikali imeshatenga maeneo maalum kwa
ajili ya shughuli za ufugaji, lakini kutokana na kiburi cha fedha
wafugaji wanawatumia baadhi ya wenyeviti na watendaji wa serikali za
vijiji wasiokuwa waaminifu kukahidi na kupeleka mifugo kwenye maeneo
waliyotengewa.
Dkt Ndumbaro amewaonya wenyeviti na watendaji wa vijiji hao kujiepusha
na vitendo vya rushwa kwa kupokea fedha na kuruhusu wafugaji kufanya
shughuli zao kwenye maeneo ya utalii kwani tabia hiyo ni kukiuka
sheria za utumishi wa umma.
Waziri Ndumbaro, amewataka wananchi kuepuka kuishi kufanya shughuli
zao kwenye hifadhi kwani serikali haitahusika kulipa fidia wala kutoa
kifuta machozi kwa mtu atakayepoteza maisha,kujeruhiwa na kuharibiwa
mazao.
Alisema, ili kukabiliana na wanyama wanaovamia mashamba na kuharibu
mazao,serikali kupitia wizara ya maliasili imeanza kutoa mafunzo kwa
vijana kwenye vijiji vinavyozungukwa na hifadhi na mapori ya akiba ili
kuwajengea uwezo wa kufukuza wanyama pindi wanapofika kwenye makazi ya
watu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro
alisema,wilaya hiyo ni ya kilimo lakini changamoto kubwa kuvamiwa
na wafugaji na mifugo mingi kutoka katika maeneo mengine ya nchi jambo
lililo sababisha kutokea kwa migogoro kati ya jamii ya wafugaji na
wakulima.
Alisema, licha ya serikali ya wilaya kutenga zaidi ya vitalu 200 vya
ufugaji,lakini jambo la kusikitisha baadhi ya viongozi wa ngazi za
vijiji wanaruhusu wafugaji kupeleka mifugo kwenye maeneo
yasioruhusiwa.
Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama alisema,
katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali ya wilaya inafanya
operesheni za mara kwa mara kuwaondoa wavamizi wote wanaofanya
shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi na maeneo yote yasioruhusiwa.
Baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo,wameiomba serikali kupitia upya
viwango vya fedha vinavyotolewa kwa waathirika wa matukio ya
kushambuliwa na wanyama wakali na wanao haribu mazao kwani
havilingani na hasara inayotokea.
Mwenyekiti wa Baraza la wazee wilaya ya Tunduru Ajili Kalolo alisema,
wananchi wanalazimika kuondoa mazao yao mashambani kabla hayajakomaa
ili kuepuka kuliwa na wanyama.Kalolo alisema, kama serikali itaendelea na msimamo wake wa kuwaona
wananchi ndiyo wenye makosa kwa kile kinachodaiwa kuvamia kwenye
hifadhi basi kuna hatari wilaya hiyo kukumbwa na janga la njaa.
Msanga Rashid mkazi wa kijiji cha Kalulu, ameiomba wizara ya
maliasili kuwasaidia kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu wa
mazao,badala ya kuwaona wananchi ndiyo wakosaji kwani kama serikali
itaendelea na msimamo huo kuna hatari baadhi ya vijiji kutokuwa na
watu kwa kuuawa na wanyama.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.