Waganga Wakuu wa Mikoa wapewa Siku 30 kutathmini utendaji wa Kamati za afya za Mikoa na Wilaya-Dkt.Gwajima
Songea, 04 Aprili, 2019
Waganga wakuu wa Mikoa Tanzania Bara wamepewa mwezi mmoja kuhakikisha kuwa wanazifanyia tathmini ya kina kamati za Uendeshaji Huduma za Afya za Mikoa na wilaya zao kuona kama zinaendana na kasi ya mabadiliko yanayokusudiwa na Serikali ya awamu ya tano.
Agizo hilo limetolewa jana mjini Songea na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt.Dorothy Gwajima wakati akizungumza na wajumbe wa kamati ya Uendeshaji Huduma za Afya ya Mkoa wa Ruvuma pamoja za Halmashauri za wilaya ya Namtumbo na Songea pamoja na Manispaa ya Songea.
Amesema anawapa siku 30 Waganga wakuu wa Mikoa yote kuhakikisha kuwa wanafanya tathmini ya wajumbe waliopo katika ofisi zao kama wanatosha kuendelea na nyadhifa zao za kusimamia jukumu la uendeshaji huduma za afya katika mikoa na halmashauri zao.
Dkt Gwajima ameongeza kuwa endapo itabainika kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati hizo hawana sifa zinazowafanya kushindwa kutekeleza majukumu yao ya usimamizi na uendeshaji huduma za afya katika maeneo yao, waganga wakuu wa mikoa watalazimika kuwaweka pembeni wajumbe hao na kuunda upya kamati ambazo zitaweza kuiendeleza agenda ya mabadiliko katika sekta ya afya.
“Kinyume na hapo katika ziara hizi ninazoendelea kuzifanya mikoani nikikuta yupo Mganga Mkuu ambaye ametulia tu, mapungufu katika vituo bado yapo na amewezeshwa na serikali, ajue wazi kuwa wa kutokutosha wa kwanza atakuwa yeye,” amesema Dkt Gwajima na kuongeza:
“Haiwezekani tukute mapungufu madogo kabisa katika vituo, ambayo yangeweza kuonwa na wao walioko huko eti hayaonekani hadi tuje sisi kutoka Tamisemi ndiyo mapungufu hao yafanyiwe kazi,”amesisitiza Dkt Gwajima.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameonya tabia iliyojengeka miongoni mwa wajumbe wa kamati za uendeshaji huduma ya afya kukimbilia kuomba msamaha pindi zinaposhindwa kutekeleza majukumu yake kwa makusudi.
Amesema huu ni wakati wa kuboresha sekta ya afya katika vituo vya afya na zahanati kwa kuhakikisha kuwa mazingira ya utoaji huduma yanaboreshwa ili yaweze kuwavutia wananchi wengi kukimbilia kupata huduma katika zahanati na vituo vya afya vinavyomilikiwa na serikali.
Dkt Gwajima amesema kuwa kamwe hatawapa nafasi wajumbe wa kamati za uendeshaji huduma za afya wa mikoa na wilaya ambao siku zote wamekuwa ni watu wa visingizio vya kuomba kusamehewa ama kupewa muda kuwa wamefahamu mapungufu yao.
Amesema angependa kuona kamati za uendeshaji huduma za afya katika mikoa na halmashauri zikijikita katika kuongelea mambo makubwa yanayolenga kuishirikisha sekta na serikali kuu.
“Hivi vitu vidogo vidogo vya kitaalamu tubebe sisi wenyewe, wananchi wametuunga mkono, tumeweza kushirikiana nao kujenga zahanati na vituo vya afya katika mikoa na halmashauri zetu hivyo ni jukumu letu sasa kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bora za afya kwa wananchi,” amesema.
Kwa mujibu wa Dkt.Gwajima, katika ziara zake alizokwisha zifanya katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Njombe na Ruvuma amejionea mapungufu mbalimbali ya utoaji wa huduma bora za afya katika vituo vya afya na zahanati.
Ameongeza kuwa mapungufu hayo ambayo ameyashuhudia kwenye vituo vya afya na zahanati zinazomilikiwa na umma yametokana na watendaji hao kutopata usimamizi unaostahili kutoka kwa kamati za usimamizi na uendeshaji wa huduma za afya za mikoa na halmashauri husika.
Dkt Gwajima anaamini kuwa kushindwa kwa kamati za uendeshaji ndiko kulikopelekea kukithiri kwa uchafu katika majengo ya vituo vya afya na zahanati nchini licha ya vituo hivyo kuwa na fedha za uendeshaji wake.
Sambamba na kuwataka waganga wakuu wa mikoa kuzitathmini kamati hizo, Dkt Gwajima amewataka waganga wakuu wote kutambua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli ana agenda moja tu ya kuleta mabadiliko katika sekta ya afya.
“Hatutapimwa kwa idadi ya semina au vituo vya afya tulivyojenga bali kwa ubora wa kazi za kuhudumia wananchi,” amesema.
Dkt Gwajima amebainisha mapungufu kadhaa aliyoyaona kwenye ziara yake kuwa ni pamoja kuwepo kwa malalamiko toka kwa wagonjwa na kukosekana kwa takwimu sahihi za utendaji kazi
Akiwa katika kituo cha afya Mjimwema Manispaa ya Songea Naibu Katibu Mkuu Dkt.Gwajima alipokea kero za wagonjwa kuhusu uwepo wa kauli mbaya toka kwa wauguzi na tatizo la ukosefu dawa hususan akina mama wajawazito
“Hapa Mjimwema nimebaini kasoro nyingi mojawapo kauli mbaya za watumishi na tatizo la dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa ” Dkt .Gwajima alionya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt.Jairy Khanga ameahidi kuchukua hatua za mapema kufanya mabadiliko ya utendaji kazi wa kamati za usimamizi wa huduma za afya katika mkoa wa Ruvuma .
Mwisho.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.