WATU 496 sawa na asilimia 71 kati ya watu 696 waliofanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo kutoka vijiji mbalimbali katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wamebainika kusumbuliwa na shinikizo la juu ya Damu.
Wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa chakula wenye uhusiano wa moja kwa moja na ugonjwa wa moyo ni asilimia 37na wagonjwa 222 sawa na asilimia 32 wamegundulika kuwa na matatizo ya kisukari.
Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) Dkt Baraka Ndelwa,wakati wa zoezi la awali la uchunguzi wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu lililofanyika katika kijiji cha Luhimbalilo kata ya Mputa wilayani Namtumbo.
Amesema,wametoa rufaa kwa wagonjwa watano kwenda Hospitali ya Jakaya Kikwete kwa uchunguzi zaidi na wagonjwa wengine wamewapa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya mkoa Songea (Homso)na Hospitali ya St Joseph Peramiho.
Dr. Ndelwa ameema,katika zoezi hilo wamegundua watu wengi wanaugua magonjwa ya moyo na sukari, lakini wanashindwa kupata matibabu ya uhakika kutokana na upatikanaji wa matibabu ya kwenye ngazi ya zahanati na vituo vya afya kutokuwa rafiki.
Amesema,ugonjwa wa shinikizo la damu husababisha matatizo mbalimbali ikiwemo kiharusi,na moyo kushindwa kufanya kazi hali inayoweza kusababisha kifo kwa mgonjwa ambaye hajapata matibabu.
Dkt Ndelwa,ameshauri kuanzishwa kliniki maalum za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kwenye vituo vya afya na Hospitali za wilaya, ili kuweza kuwafuatilia kwa karibu wananchi watakaobainika kupata ugonjwa huo,na kuwawezesha watoa huduma vifaa vya kisasa vya kutolea huduma kwa wagonjwa.
Ameiomba serikali,kupeleka dawa za magonjwa ya moyo na kisukari kwenye zahanati ili ziweze kuwasaidia wananchi wengi wenye matatizo hayo,badala ya kuishia kwenye Hospitali za rufaa za mkoa ambako upatikanaji wake ni rahisi.
Muuguzi kutoka Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) Silvia Millanzi alisema,watu wengi waliojitokeza kwenye kambi za uchunguzi na matibabu katika kituo cha afya Lusewa,Hospitali ya wilaya Namtumbo na kituo cha afya Mputa wanafahamu hali za afya zao.
Hata hivyo,changamoto kubwa ni kutofuatilia matibabu kutokana na hali ya kiuchumi au upatikanaji wa dawa kwenye maeneo yao,jambo ambalo ni hatari kwa sababu mgonjwa asiyepata matibabu anaweza kupata magonjwa mengine hatari ikiwemo figo.
Millanzi,ameiomba jamii hasa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa shikinikizo la damu,kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya wataalam kuhusu umuhimu wa kutumia dawa hizo kila siku katika maisha yao, ili kuzuia madhara zaidi yanayoweza kutokea.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.