Mradi wa AIDI TANZANIA umegawa mizani iliyounganishwa na mfumo wa simu na vishikwambi ambayo itatumika kwenye vituo vya kukusanyia mazao mkoani Ruvuma ili kuhakikisha mkulima kupata kilo halali kwenye mazao yake.
Meneja wa mradi wa AIDI na Mkurugenzi wa Rotai Company Limited Felix Awino amesema hayo wakati anazungumza kwenye hafla fupi ya ugawaji wa vishikwambi na Mizani ya kieletroniki katika ukumbi wa Mipango uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
Awino amesema katika Mkoa wa Ruvuma wanalenga kuingiza mazao ya mahindi maharage na Soya kwenye mfumo rasmi wa mauzo ya kidigitali na kwamba ili mkulima atumie mzani itamlazimu awe amesajiliwa.
"Mradi wa AIDI upo Kwa lengo la kuendeleza wakulima kwenye mfumo wa kijiditali na kwamba tumedhamiria kuhakikisha wakulima wadogo wanapata masoko ndani na nje ya nchi Kwa kupitia mifumo ya kidigitali", Amesema Awino.
Katika hafla hiyo wagani kazi 15 wamegawiwa vishikwambi ambapo AIDI imekusudia kuwafikia wagani kazi 300 waliopo Mkoani Ruvuma ambao watapata mafunzo ya namna ya kusajiri na kukusanya mazao Kwa njia ya kidigitali na mawasiliano ya anga.
Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Jumanne Mwankhoo amezitaja faida za mfumo huu, kuwa utasaidia wakulima kupata huduma za ugani katika sehemu ambazo hazina maafisa ugani kwa kuwa una upungufu wa maafisa ugani 600.
Amesisitiza kuwa Mradi huo utaongeza uhakika wa usalama wa chakula kutokana na kuongezeka Kwa tija katika uzalishaji na kwamba amewashauri maafisa ugani waliopewa vifaa hivyo wavitunze na kuhakikisha vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa BRITEN, Ainea Mgulambwa amesema wamejikita katika kuboresha mtandao wa usambazaji wa pembejeo ususani maeneo ya vijijini ili mkulima asipate shida ya kutembea umbali mrefu kufuata pembejeo.
Naye Afisa Mipango Soko la Bidhaa Tanzania, Eva Msangi ameitaja kazi kubwa ya Taasisi yake ni kukutanisha wauzaji na wanunuzi wa bidha Kwa kutumia mfumo wa kielectroniki na kuhakikisha ununuzi na ushindani wa bei katika masoko.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Afisa Udhibiti Ubora Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala ( WRRB) Witness Temba amesema kupitia mfumo wa Stakabadhi Ghala wakulima na vyama vya ushirika vya msingi wanaweza kukusanya mazao yao katika maghala na wakapatiwa Stakabadhi ambayo imebeba taarifa zote kuhusu mzigo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.