WAKULIMA mkoani Ruvuma wameuza jumla ya kilo milioni 3,836,889 za zao la ufuta kwa bei ya wastani wa shilingi 3,652.00 kwa kilo kupitia stakabadhi ya ghala kwa kutumia mfumo wa TMX.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati anatoa salamu za Mkoa kwa Naibu Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye amefanya ziara ya kikazi ya siku moja wilayani Songea.
Amesema wakulima hao wameuza ufuta katika minada iliyofanyika katika wilaya za Namtumbo,Songea na Tunduru ambapo ameipongeza Wizara yenye dhamana ya teknolojia kwa kuwezesha utumiaji wa mfumo katika eneo la uuzaji wa mazao kwa njia ya stakabadhi za ghala.
Hata hivyo amesema wakulima mkoani Ruvuma msimu huu katika zao la mahindi wanatarajia kuvuna tani milioni 1,882,473 ,uzalishaji ambao umechangiwa kwa kiasi kikubwa na upatikanaji wa mbolea ya ruzuku.
“Mkoa wetu hivi sasa unashika nafasi ya nne kitaifa kiuchumi,Pamoja na jitihada za wananchi wetu ambao wanajishughulisha na shughuli za kilimo lakini uwekezaji uliofanywa katika makaa ya mawe unachangia Zaidi katika ukuaji wa uchumi katika Mkoa wetu’’,alisisitiza Kanali Abbas.
Mkuu wa Mkoa ameyataja mafanikio mengine katika sekta za huduma za jamii ambapo katika sekta ya elimu,Mkoa umeweza kupokea wanafunzi wote wanaoanza kidato cha kwanza kwa mara moja.
katika eneo la afya Kanali Abbas amesema Mkoa pia umepiga hatua kubwa ikiwemo ya kuwa na mashine ya kisasa ya CT-Scan jambo ambalo limerahisisha matibabu ya wagonjwa na kwamba mfumo wa matibabu umekuwa wa kidigitali.
Kuhusu Sekta ya umeme Kanali Abbas amesema,Mkoa umepata mafanikio makubwa ambapo vijiji 541 kati ya 554 vimeunganishwa na umeme sawa na asilimia 97.7
Akizungumzia eneo la sekta ya mawasiliano, amesema eneo kubwa la Mkoa wa Ruvuma lina mawasiliano ya simu na kwamba kuna maeneo machache ambayo hayana mawasiliano.
Kwa upande wake Meneja TTCL Mkoa wa Ruvuma Zabron Magabula amesema serikali inatarajia kujenga minara nane ya mawasiliano katika Mkoa wa Ruvuma ambayo itaunganishwa na mkongo wa Taifa ili kupanua wigo na kuboresha mawasiliano ya intaneti na sauti.
Amesema ndani ya kipindi cha siku 50 serikali itajenga minara miwili ya mawasiliano katika vijiji vya Maposeni na Mdunduwaro wilayani Songea kwa gharama ya takribani shilingi milioni 600 ili kuboresha mawasiliano.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema serikali imedhamiria kusogeza huduma ya mawasiliano ya uhakika kwa wananchi kwa kuwa nchi inahitaji uchumi wa kidijitali.
Amesema serikali inaufanya Mkoa wa Ruvuma kuwa miongoni mwa mikoa inayokuwa katika teknolojia ya kidigitali ambapo amekagua maeneo ya Maposeni na Mdunduwaro ambako serikali imetoa fedha za kujenga minara miwili ya mawasiliano inayounganishwa na mkongo wa Taifa.
Naibu Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi akizungumza na wananchi wa Maposeni wilayani Songea
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.