Wakulima wa Mbaazi Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wameingiza katika mzunguko zaidi ya bilioni 3.7 katika zao la Mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani
Mnada wa tatu wa uuzaji wa Mbaazi uliofanyika kijiji cha Angalia Kata ya Mtina,katika ofisi za Chama cha Ushirika cha Mshikamano ulikuwa na mafanikio makubwa. Jumla ya tani 1928 za Mbaazi ziliuzwa katika mnada huo, ambazo ni sawa na kilo milioni 1.9.
Idadi ya wanunuzi katika mnada huo ilikuwa 20, hata hivyo ni wanunuzi 6 tu ndio ambao walikaribia bei iliyotarajiwa na wakulima. bei ya juu ilikuwa shilingi 1,950 na kufanya bei wastani kuwa shilingi 1,946. Wakulima walikubali kuuza Mbaazi kwa bei ya wastani ya shilingi 1,948. Hii inaonyesha kuwa uuzaji ulikuwa na ushindani mkubwa kati ya wanunuzi.
Aidha Mlajisi Msaidizi vyama vya Ushirika mkoa wa Ruvuma Bi. Peja muhoja amewasisitiza wakulima wa mazao yote ya biashara kuacha kuuza mazao yao kwa mtu kati (mlanguzi), na kuwataka kutumia mfumo wa Stakabadhi ghalani wenye manufaa makubwa kwa mkulima.
"Zao la Mbaazi limekuja na bei nzuri ,wakulima wakaongeze juhudi shambani, mashamba mapya na wayapande katika utaratibu wa kuzingatia kanuni bora za kilimo, vile vile fedha wanazozipata wakazitumie vyema kwa maendeleo yao Binafsi”. Alisema.
Pia kwa upande wake mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika Tunduru Ndg. Mussa Manjaule amewasisitiza wakulima kuzidi kutanua na kuwekeza zaidi katika kilimo ,pia amewasisitiza wakulima kulima mazao mbalimbali mbadala ya chakula,kutokujikita kwenye zao la aina moja tu.
Zao la Mbaazi limepanda thamani katika soko ukilinganisha na kipindi cha nyuma, ambapo lilikua likionekana kama zao la chakula pekee,lakini kwa sasa limeingia katika mkakati wa kibiashara kwa kuuzwa zaidi ya shilingi 1,500. Bei hii inaweza kuwa chanzo cha kuridhika kwa wakulima na inaweza kuwachochea kuendelea kulima Mbaazi kwa wingi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.