Wakulima wa kahawa katika Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, wameeleza kuridhishwa na mpango wa serikali wa kutoa pembejeo za ruzuku kwa misimu ya kilimo ya 2023/2024 na 2024/2025,Hatua iliyochangia kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo.
Kupungua kwa bei ya mbolea kumewawezesha wakulima kupata pembejeo kwa gharama nafuu, hali inayochochea maendeleo ya sekta hiyo.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa Mbinga (MBIFACU), Michael Kanduyu, amesema kuwa ruzuku hiyo imepunguza bei ya mbolea, ambapo UREA sasa inauzwa Sh. 68,000, CAN Sh. 62,000 na SA Sh. 48,000, ikilinganishwa na bei ya awali ya Sh. 150,000 hadi Sh. 180,000 kwa mfuko mmoja.
Ameitaka serikali kupanua mpango huo kwa dawa za kupulizia kahawa ili kupunguza zaidi gharama za uzalishaji.
Lucas Mahay, mkulima kutoka Kijiji cha Malindindo, amesema kuwa kabla ya mpango wa ruzuku, wakulima walilazimika kupunguza ukubwa wa mashamba yao kutokana na gharama kubwa za pembejeo. Hata hivyo, mpango huu umewasaidia kurejesha matumaini na kupanua mashamba yao. Pia, amesifu hatua ya Mbifacu kuanzisha mfumo wa mikopo ya mbolea kwa wakulima, ambao umeongeza ushiriki wao katika vyama vya ushirika.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mbifacu, Faraja Komba, amesema kuwa uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka wastani wa tani 15,000 msimu wa 2021/2022 hadi tani 25,000 msimu wa 2024/2025. Ongezeko hilo limewanufaisha wakulima kwa mapato zaidi na kuchangia katika pato la serikali kupitia ushuru na tozo mbalimbali.
Pia, vyama vya ushirika vimewekeza katika miradi ya maendeleo kama mashamba, vyombo vya usafiri na maghala ya kuhifadhi kahawa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.