BENKI ya NMB imezindua kampeni ya Bonge la Mpango Mchongo wa kilimo katika Kanda ya Kusini ambapo wakulima watano na Chama kimoja cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wameshinda.
Uzinduzi huo katika Kanda ya Kusini ulifanyika jana katika soko kuu la mjini Namtumbo mkoani Ruvuma ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya aliyewakilishwa na Msyangi Kuruchumila.
Mwakilishi wa Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Roman Degeleki aliwataja wakulima watano walioshinda shilingi 100,000 kila mmoja kwenye droo ya wiki hii katika kampeni hiyo kuwa ni Alex Nombo wa Litembo Mbinga,Melina Saanze wa Mtwara,Malongo James wa Songea,Mustapha Milanzi wa Nanyumbu Mtwara na Hamidu Omary wa Mtwara.
Alikitaja Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) ambacho kimejinyakulia pikipiki kwenye mchongo wa kilimo kuwa ni Rwinga AMCOS ya mjini Namtumbo mkoani Ruvuma.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo,Meneja huyo wa Kanda alisema NMB imeamua kuzindua kampeni kabambe ya bonge la mpango mchongo wa kilimo awamu ya pili katika kanda ya kusini,ambapo AMCOS na wakulima watakaoweka akiba kupitia akaunti zao za NMB wataingia kwenye orodha ya wanaostahili kujishindia fedha taslimu,pikipiki za miguu miwili na miguu mitatu.
“Kwenye kampeni hii zaidi ya shilingi milioni 40 zitatolewa kama zawadi kwa washindi zaidi ya 50,kampeni itaendeshwa ndani ya wiki tano,kila wiki wakulima watano watapokea shilingi 100,000 kila mmoja na AMCOS moja itajinyakulia pikipiki’’,alisisitiza.
Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya ameupongeza uongozi wa NMB kwa kuamua kuleta kampeni ya Bonge la Mpango mchongo wa kilimo katika wilaya ya Namtumbo yenye wakulima wengi wanaozalisha mazao mbalimbali kama vile mahindi,ufuta,soya,korosho na mpunga.
Malenya ametoa rai kwa wakulima wa Namtumbo kuchangamkia fursa waliopewa na NMB kwa kuweka akiba na kufungua akaunti mpya ili kuanza kuweka akiba na kujishindia zawadi mbalimbali kutoka NMB.
“Ndugu zetu wa NMB wameenda hatua kubwa zaidi mbele,akiba unaweka kwa ajili yako,inabaki kuwa fedha yako,lakini wao wanakupa zawadi kwa kuwa umeamua kufungua akaunti na kuweka akiba,hili ni jambo kubwa sana,NMB wanastahili pongezi’’,alisisitiza Malenya.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa funguo za pikipiki kwenye uznduzi huo, kiongozi wa AMCOS ya Rwinga Mohamed Komba aliwapongeza NMB kwa kutoa zawadi ya pikipiki katika AMCOS hiyo baada ya kushinda ambapo alisema itawarahishia kuwatembelea na kuwafikia wakulima kwa urahisi hivyo kuongeza tija kwenye kilimo.
Naye Rashid Abdalah Mkulima wa Namtumbo ametoa rai kwa Benki ya NMB kutoa mikopo ya aina mbalimbali yenye riba nafuu kwa wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.