WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Mataka kata ya Mchangani katika Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,wameiomba serikali kukamilisha haraka ujenzi wa bweni ili kuwaondolea kero ya kulala katika vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Mataka.
Wakizungumza mbele ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Hairu Musa wamesema,kuendelea kulala kwenye madarasa inawasababishia kukosa muda wa kujisomea hasa nyakati za usiku kutokana na kuwepo kwa matukio ya wizi yanayofanywa na vijana kutoka mtaani.
Omari Rashid wa kidato cha tano amesema, kukosekana kwa ulinzi kunapelekea kutumia muda mwingi kujilinda na kulinda vifaa vyao kama hatua ya kukabiliana na matukio hayo yanayotokea mara kwa mara.
Orestus Masoud amesema,matukio ya wizi yanayofanywa na watu wasiofahamika yanawanyima nafasi ya kuzingatia yale yanayofundishwa na walimu kwa sababu wanajikuta wanasinzia wakiwa darasani.
Amesema,hali hiyo inatokana na muda wa usiku wanaotakiwa kupumzika kujilinda na waharifu hao wanaotoka katika maeneo mbalimbali ya mji wa Tunduru na kuiomba serikali kuongeza fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio kuzunguka eneo lote la shule.
Mkuu wa shule hiyo Niver Mbunda amesema,wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kwa kushirikiana na Diwani wa kata ya Mchangani Hairu Musa wamechanga Sh.milioni nne kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80.
Aidha amesema,Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Kungu katika kuunga mkono jitihada za wazazi kupitia mfuko wa Jimbo amechangia mifuko 600 ya saruji ambayo imesaidia kukamilisha boma na mwezi April mwaka huu Serikali imetoa Sh.milioni 80 ili kukamilisha ujenzi huo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mchangani Hairu Musa amesema,lengo la kujenga bweni hilo ni kuwezesha wanafunzi wa kidato cha tano na sita kuwa na sehemu nzuri na salama ya kuishi na kuwaondolea changamoto ya kukaa kwenye madarasa ya shule ya msingi ambayo hayana ubora.
Hairu ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Tunduru amesema,wanahitaji zaidi ya Sh.milioni 130 kukamilisha kazi hiyo na kuiomba Serikali na wadau wengine kuendelea kuwaunga mkono kwa kuchangia fedha na vifaa vitakavyotumika kukamilisha ujenzi wa bweni na kujenga uzio kuzunguka eneo lote la shule.
Ameeleza kuwa,Halmashauri ya wilaya Tunduru kwa kushirikiana na wazazi,jamii na wadau mbalimbali wameanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa mabweni katika shule zote za sekondari kwa ajili kuwawezesha wanafunzi kuishi shuleni ili wapate muda mwingi zaidi wa kujisomea hasa nyakati za usiku hatua ambayo itasaidia sana kuinua kiwango cha taaluma katika wilaya hiyo kongwe hapa nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.