Zaidi ya wananchi 900 wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani bila malipo katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho, mkoani Ruvuma, kupitia kambi maalum ya siku nne iliyohusisha madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road.
Akizungumza wakati wa ziara yake hospitalini hapo, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kambi hiyo inalenga kutoa huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti, tezi dume na aina nyingine, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kupambana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
“Takwimu zinaonesha watu 18 wamekutwa na viashiria vya saratani; kati yao wanawake 12 tayari wameanza matibabu na wanaume sita wamepewa rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” amesema Waziri Mhagama na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha huduma hizo muhimu kwa wananchi.
Ameongeza kuwa utafiti wa Tume ya Saratani (Oncology Commission Report) unaonesha kuwa ifikapo mwaka 2030, idadi ya vifo vitokanavyo na saratani katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inaweza kuongezeka hadi kufikia watu milioni moja iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Akitaja aina za saratani zinazoongoza hapa nchini, Mhagama amesema kuanzia mwaka 2019 hadi 2024, saratani ya mlango wa kizazi inaongoza kwa asilimia 41, ikifuatiwa na saratani ya matiti kwa asilimia 19, utumbo mkubwa na mdogo asilimia 6.1, koo asilimia 5.7 na saratani ya kichwa na shingo kwa asilimia 4.3.
Amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuzingatia ulaji bora, kuepuka vyakula vyenye mafuta, chumvi,sukari nyingi, kuacha matumizi ya vilevi, na kupima afya zao mara kwa mara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Ocean Road, Dkt. Diwani Msemo amesema taasisi hiyo imeamua kuwachukua wataalamu wanne kutoka Peramiho kwa ajili ya mafunzo maalum, ili waweze kutoa huduma za saratani kwa ufanisi zaidi pindi watakaporejea hospitalini hapo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.